1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Besigye awekwa katika kifungo cha nyumbani

20 Februari 2016

Vikosi vya usalama nchini Uganda Jumamosi (20.02.2016) vimemuweka katika kifungo cha nyumbani mgombea mkuu wa upinzani kuzuwiya kuongoza maandamano ya upinzani wakati nchi ikisubiri matokeo ya uchaguzi uliozusha utata.

https://p.dw.com/p/1Hz1W
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye.
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye.Picha: MICHELE SIBILONI/AFP/Getty Images

Vikosi vya usalama nchini Uganda Jumamosi (20.02.2016) vimemuweka katika kifungo cha nyumbani mgombea mkuu wa upinzani kuzuwiya kuongoza maandamano ya upinzani wakati nchi hiyo ikisubiri matokeo ya uchaguzi uliozusha utata.

Msemaji wa polisi Fred Enaga ameliambia shirika la habari la AP kwamba polisi imechukuwa hatua za kinga dhidi ya Kizza Besigye kuzuwiya machafuko zaidi.

Polisi hapo Ijumaa iliyazingira makao makuu ya chama cha Besigye cha FDC wakati Besigye alipokuwa akikutana na wanachama wa chama chake na helikopta ilifyatuwa gesi ya kutowa machozi kwa umma uliokusanyika nje.

Polisi baadae ilimchukuwa Besigye daktari huyo mwenye umri wa miaka 59 na kumpeleka sehemu isiojulikana ambapo baadae usiku ilimweka katika kifungo cha nyumbani.

Tume ya uchaguzi yalaumiwa

Wangalizi wa kimataifa walioshuhudia mchakato wa uchaguzi nchini Uganda wamelimbika lawama kwa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ,vyombo vya usalama pamoja na vyama vya kisiasa kwa kile walichokitaja kupuuzilia masuala nyeti ambayo yangepelekea kiwango bora cha zoezi huru na la haki la uchaguzi.

Polisi ikimshikilia mfuasi wa Bessigye nje ya ofisi yake Kampala. (19.02.2016)
Polisi ikimshikilia mfuasi wa Bessigye nje ya ofisi yake Kampala. (19.02.2016)Picha: Reuters/G. Tomasevic

Wakitoa taarifa zao za awali, wangalizi kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki,COMESA na IGAD hata hivyo wamewapongeza wapiga kura kwa kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kidemokrasia.

Kwenye kikao kilichojumuisha makundi ya wangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki,Jumuiya Maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika IGAD pamoja na Jumuiya ya ushirikiano wa kibiashara COMESA wakuu wa ujumbe wa wangalizi walielezea masikitiko yao kuhusu mapungufu kadhaa yaliyotatiza zoezi la uchaguzi na kuwatia wasi wasi wapiga kura na mashaka kama wangeliweza kupiga kura.

Kasoro za uchaguzi

Suala kuu lilikuwa kuchelewa kuwasilishwa kwa vitendea kazi na kwamba kule vilikofikishwa vilikuwa havitoshi hiki ndicho kilikuwa chanzo cha rabsha zilizozuka na baadaye tume hiyo ikalazimika kuongeza muda wa kupiga kura hadi usiku na jambo lililoleta mashaka kuhusu usalama wa watu na kura zao. Wangalizi hao waliokwenda sehemu mbalimbali za nchi aidha wamekosoa tume hiyo kwa kutofanya uhamasishaji wa kutosha pamoja na mafunzo kwa maafisa.

Hadi tukienda hewani tume ya uchaguzi imetangaza matokeo kutoka asilimia 82. na rais Museveni angali anaongoza kwa kura 5,047,754 sawa na aslimia 61.55; Besigye amepata kura 2,826,644 huku Amama Mbabazi akiendelea kufanya vibaya akiwa na kura 122,848.

Polisi ikimpiga mfuasi wa Bessigye Kampala. (19.02.2016)
Polisi ikimpiga mfuasi wa Bessigye Kampala. (19.02.2016)Picha: Reuters/G. Tomasevic

Lakini wangalizi wana mtazamo kwamba mchakato wa kuwasilisha matokeo huelezei kwa undani kule yanakotoka matokeo na hivyo kutoaminiwa na wapiga kura.Mwendo wa saa kumi waganda watakuwa wamejua mshindi katika uchaguzi kile kinachobaki Ni jinsi matokeo hayo yatajavyopokelewa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Lubega Emmanuel

Mhariri : Mohamed Dahman