1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Besigye azidi kuonja joto la jiwe Uganda

19 Februari 2016

Vikosi vya usalama vya rais Yoweri Museveni vimetumia nguvu katikati mwa uchaguzi siku ya Ijumaa, na kumkamata mgombea mkuu wa upinzani, kuwapiga waandamanaji na kuwafyatulia mabomu ya machozi na magruneti ya kuzimia.

https://p.dw.com/p/1HysE
Vikosi vya usalama vimeshtumiwa kwa kumnyanyasa mgombea wa upinzani Kizza Besigye.
Vikosi vya usalama vimeshtumiwa kwa kumnyanyasa mgombea wa upinzani Kizza Besigye.Picha: Reuters/J. Akena

Marekani, ambayo inatoa msaada wa kifedha kwa Uganda na kulisaidia jeshi lake, ilikuwa miongoni mwa waliolaani vitendo hivyo vya kinyama. Ubabe huo ulitokea wakati zoezi la uchaguzi likiendelea katika wilaya mbili muhimu siku ya Ijumaa kutokana na kutofika kwa karatasi za kura na vidaa vingine vy auchaguzi kama ilivyokuwa imepangwa siku ya uchaguzi.

Matokeo ya mwanzo yalimuonyesha Museveni akiwa mbele ya kiongozi wa upinzani Kizza Besigye, lakini kura zilikuwa bado hazijapigwa na kuhesabiwa katika ngome za Besigye. Wakati matokeo kutoka asilimia karibu 23 ya vituo yakiwa yamekwisha hesabiwa, Museveni alikuwa na asilimia 62 ya kura na Besigye alikuwa na asilimia 33, ilisema tume ya uchaguzi.

Polisi iliyazingira makao makuu ya chama cha Besigye cha Forum for Democratic Change FDC, wakati akijiandaa kukutana na viongozi wengine wa chama chake, ambapo polisi ilitumia helikopta kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi watu waliokuwa nje ya makao hayo katika eneo la Najjanankumbi, nje kidogo ya jiji la Kampala.

Polisi ilimkamata Besigye na viongozi wenzake wa FDC na kuwapeleka kusikojulikana.
Polisi ilimkamata Besigye na viongozi wenzake wa FDC na kuwapeleka kusikojulikana.Picha: Reuters/J. Akena

Baadaye polisi iliingia ndani ya makao hayo na kumkamata Besigye pamoja na rais wa chama hicho Jenerali mstaafu wa jeshi na mkuu wa zamani wa jeshi la UPDF Mugisha Muntu pamoja na mwenyekiti wa taifa wa chama Wasswa Biriggwa, na kuwapaleka katika eneo lisilojulikana, kulingana na Semujju Ibrahim Nganda, msemaji wa chama cha FDC.

Marekani yakaripia

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, alizungumza kwa njia ya simu na Museveni siku ya Ijumaa "kusisitiza kwamba maendeleo ya Uganda yanategemea kuheshimu kanuni ua demokrasia katika mchakato wa uchaguzi unaoendelea," ilisema taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Kerry "alieleza wasiwasi wake kuhusiana na kukamatwa na kuzuwiwa korokoroni kwa Besigye...na unyanyasaji wa wanachama wa vyama vya upinzani wakati wa zoezi la kupiga kura na kujumlisha matokeo, na kumtaka rais Museveni kuvidhibiti vikosi vya jeshi na polisi."

Ubalozi wa Marekani ulisema katika mtandao wa Twitter kwamba "Tunalaani vikali matumizi ya nguvu iliyopitiliza na polisi leo katika makao makuu ya FDC mjini Kampala."

Baada ya kukamatwa kwa Besigye, wafausi wake waliokuwa ndani ya jengo la makao makuu waliungana na wafuasi wa Besigye walioko mitaani. Polisi wa kutuliza ghasia waliwarushia mabomu ya kutoa machozi na magruneti ya kupoteza fahamu, na pia kufyatua hewani risasi za moto kablaya kuwakamata baadhi yao.

Katika maeneo maskini ya jirani, watu waliweka vizuwizi vya moto njiani, ambavyo viliondolewa haraka na jeshi kwa kusaidiana na polisi. Waandamanaji wenye hasira pia waliweka vizuwizi vya mawe katika barabara ya kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe.

Askari jeshi wakimburuta mfuasi wa Besigye mjini Kampala.
Askari jeshi wakimburuta mfuasi wa Besigye mjini Kampala.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Muthoni Wanyenki, mratibu wa kanda wa shirika la haki za binaadamu la Amnesty International, alibainisha kwamba uvamizi huo wa vikosi vya usalama dhidi ya ofisi za FDC unawakilisha "ukandamizaji dhidi ya haki ya uhuru wa kuwa na chama na kukusanyika. Vikosi vya usalama vifanye kazi kw akujizuwia."

Polisi waliegesha magari yao karibu na nyumbani kwa mfombea urais mwingine Amama Mbabazi, waziri mkuu wa zamani. Msemaji wake Josephine Mayanja Nkanji, alisema kuwa Mbabazi alitafsiri upelekaji huo wa vikosi vya polisi kuwa hawezi kuondoka nyumbani kwake.

Museveni aongoza, mawaziri wake chali

Uchaguzi uliyofanyika siku ya Alhamisi ulikumbwa na ucheleweshwaji wa vifaa vya uchaguzi, hasa katika maeneo yanaoonekana kuwa ngome za upinzani, na hili lilichukuliwa na wapinzani kuwa ni maksudi. Upigaji kura ulikuwa unafanyika siku ya Ijumaa katika vituo 36 mjini Kampala na katika wilaya jirani ya Wakiso.

Wakati Museveni akiendelea kuongoza kinyanganyiro cha urais, mawaziri wake wasiopungua 17 wamepoteza nafasi zao za ubunge, wakiwemo waziri wa ulinzi Crispus Kiyonga -- anaeongoza juhudi za kikanda kumaliza mgogoro wa Burundi --- na mwanasheria mkuu Fred Ruhindi.

Serikali iliifunga mitandao ya kijamii kama vile Twitter na Facebook lakini Waganda wengi walikwepa udhibiti huo kwa kutumia mitando ya kibinafsi maarufu kama VPN. Besigye pia alikamatwa kwa muda mfupi siku ya Alhamisi jioni baada ya kutembelea nyumba moja mjini Kampala ambako alishuku kulikuwepo na uchakachuaji wa kura uliyokuwa unaendelea.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: dpa

Miaka 30 na bado

Polisi ilisema nyumba hiyo ilikuwa kituo cha usalama na kumtuhumu Besigye kwa kuingia katika eneo la serikali bila ruhusa. Museveni mwenye umri wamiaka 71, alitwa madaraka mwaka 1986 baada ya kupigana vya mistuni kwa miaka mitano.

Ni mshirika muhimu wa Marekani katika masuala ya usalama hasa nchini Somalia. Wakosoaji wake wana wasiwasi huenda akataka kuwa mtawala wa maisha, na wanamtuhumu kwa kutmia vikosi vya usalama kuwatishia na kuwanyanyasa wapinzani.

Besigye mwenye umri wa miaka 59, alikuwa daktari binafsi wa Museveni wakati wa vita vya msituni, na alikuwa naibu waziri wa mambo ya ndani katika baraza la kwanza la Museveni. Alifarakana na rais mwaka 1999, akisema Museveni hakuwa tena anaheshimu demokrasia.

Viongozi kadhaa wengine wa Kiafrika, wakiwemo wa Zimbabwe, Angola na Rwanda wamekaa pia madarakani kwa mihula mingi, na kusababisha chuki mingoni mwa raia ambao wanahisi wamepitiliza ukaaji wao, wakitumia mamlaka yao kusalia madarakani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Suidi Mnette