1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bi Lucy Kibaki ampiga kofi msimamizi mkuu wa sherehe katika ikulu

13 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cb6x

Sherehe ya kutoa tunzo za rais iliyofanyika jana katika ikulu ya rais mjini Nairobi Kenya, ilitatizwa wakati mke wa rais Kibaki, Bi Lucy Kibaki alipompiga kibao msimamizi mkuu wa sherehe hiyo.

Msimamizi huyo, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika ofisi ya rais, aliondolewa upesi kutoka ikulu na maafisa wa usalama.

Rais Mwai Kibaki, makamu wake Moody Awori, baadhi ya mawaziri na wanadiplomasia kadhaa waliokuwa waliohudhuria sherehe hiyo, walifedheheshwa na kitendo hicho cha bi Lucy.

Msimamizi mkuu wa sherehe hiyo alikuwa ameanza kuwakaribisha wageni wakati wa ufunguzi rasmi wa sherehe hiyo inayofanyika kitamaduni baada ya sherehe za sikukuu ya Jamhuri na kumuita bi Lucy Kibaki kuwa Lucy Wambui. Lakini kabla afisa huyo kuweza kuendelea na maelezo yake, mama Lucy alisimama kutoka alipokuwa ameketi na kumwendea kwa haraka na kumchapa kibao usoni.

Sherehe hiyo ilitatizwa kwa muda mfupi wakati maafisa wa uslaama walipokuwa wakimuondoa afisa huyo aliyejawa na hofu kubwa na kumuacha kiongozi wa idara ya huduma za umma, balozi Francis Muthaura, aongoze sherehe hiyo.

Wakati huo huo, maafisa wa usalama wa ikulu ya rais waliwapokonya waandishi wa habari kamera zao na kuharibu picha walizokuwa wamepiga kabla kuzirudisha kamera hizo.