1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden asema hataifunga nchi licha ya maambukizi kuongezeka

John Juma
20 Novemba 2020

Licha ya kuongezeka kwa maambukizi ya corona, Biden amesema hataifunga nchi kabisa bali atahimiza utaratibu wa kitaifa wa watu kuvaa barakoa.

https://p.dw.com/p/3lbGn
USA Joe Biden mit Atemschutzmaske in Wilmington, Delaware
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

 

Marekani ndiyo inaongoza katika idadi ya maambukizi pamoja na vifo kutokana na COVID-19, ikiwa imeripoti zaidi ya vifo vya watu robo milioni. Hadi sasa, maambukizi yameripotiwa katika zaidi ya nchi 210 tangu visa vya kwanza viliporipotiwa nchini China Disemba mwaka 2019. 

Rais mteule wa Marekani Joe Biden amesema hataifunga nchi kabisa kutokana na corona bali atahimiza utaratibu wa kitaifa wa uvaaji barakoa. Alisema hayo baada ya kufanya mazungumzo ya Pamoja na magavana wa majimbo 10 siku ya Alhamisi.

Tangu kuzuka kwa janga la COVID-19, jumla ya watu milioni 56.54 wameripotiwa kuambukizwa virusi hatari vya ugonjwa huo ulimwenguni kote na 1,354,227 wamefariki. Hayo ni kwa mujibu wa ujumuishaji wa takwimu uliofanywa na shirika la habari la Reuters.

Maambukizi India yapindukia milioni 9

India ni taifa la pili kuathiriwa zaidi na janga la virusi vya corona. Mnamo Ijumaa, jumla ya maambukizi yaliyothibitishwa nchini humo yalipindukia milioni tisa, hospitali katika mji mkuu New Delhi zinazidi kulemewa huku makaburi yakianza kujaa. Kulingana na takwimu za hivi karibuni, zaidi ya watu 132,000 wamefariki India kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Nchi ya Urusi imerekodi idadi ya juu ya maambukizi kwa siku moja ikiwa ni jumla ya watu 23,610 hivyo kufanya takwimu za maambukizi nchini humo kupindukia milioni mbili. Aidha mnamo siku ya Alhamisi pekee jumla ya vifo 463 viliripotiwa na kufanya idadi ya vifo kuongezeka hadi 34,850 kutokana na corona.

Urusi ni taifa la tano miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi baada ya Marekani, India, Brazil na Ufaransa.

Finnland Corona-Pandemie | Drive-in-Test
Picha: Heikki Saukkomaa/Lehtikuva/imago images

Maambukizi Ujerumani yaongezeka
Nchini Ujerumani, idadi ya maambukizi iliongezeka na watu 23,648 hadi kufikia 879,564. Hayo ni kulingana na data kutoka kituo cha kudhibiti maradhi cha Robert Koch siku ya Ijumaa. Takwimu hizo zimeonesha pia kwamba watu 260 zaidi pia wamekufa hivyo kufanya idadi ya vifo kufikia 13,630.

Maafisa nchini humo, wanatoa miito ya marufuku kutangazwa dhidi ya fashifashi za kukaribisha mwaka mpya. Mwenyekiti wa vyama viwili vikuu vya polisi Rainer Wendit ameliambia gazeti la the Bild kwamba mkesha wa mwaka mpya huwa ni sherehe watu wengi huja pamoja na watu hunywa pombe, na kuzuia hali kama hiyo isitokee itapunguza uwezekano wa maambukizi zaidi.

Wakati huo huo, katika jimbo la North Rhine-Westphalia, waziri wa mambo ya ndani Herbert Reul ametaka sherehe kuendelea kuwa chache kabisa.
Mnamo siku ya Alhamisi, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, alisema huenda Umoja huo ukaidhinisha chanjo mbili dhidi ya corona ambazo zinafanyiwa majaribio sasa za kampuni ya Pfizer-BioNtech na Moderna kabla ya mwisho wa mwezi wa Disemba.

Symbolbild I elbow bump Begrüßung
Wafanyakazi wa afya wakisalimiana kwa mtindo mpya Picha: Westend61/Imago Images

Maambukizi Afrika yapindukia milioni 2
Barani Afrika, maambukizi ya corona yamepindukia milioni mbili. Hayo ni kwa mujibu wa kituo cha Afrika cha kudhibiti maradhi, kikiongeza kwamba takwimu zao zinaonesha zaidi ya watu 48,000 wamefariki kutokana na COVID-19.

Nchini Uingereza, zipo dalili kwamba idadi ya maambukizi inapungua kufuatia masharti yaliyoko sasa ya kufunga baadhi ya maduka, migahawa na kumbi za starehe. Waziri wa Afya nchini humo Matt Hancock amesema hayo, hatua inayolegeza vikwazo kuelekea msimu wa Krismasi. Akizungumza na kituo cha televisheni cha Sky News, Hancock ameongeza kuwa tayari wanayafanyia kazi masharti yatakayotumika msimu wa Krismasi.

Hong Kong yaahirisha masomo ya wanafunzi

Nchini Hong Kong, maafisa wameahirisha masomo katika madarasa ya chini ya shule za msingi, baada ya afisa mkuu wa afya wa mji huo kusema kuwa maambukizi ya corona yanaendelea kuwa mabaya zaidi.

Masomo ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu yatasitishwa kwa wiki mbili kuanzia Jumatatu. Hatua hiyo inajiri baada ya masomo ya wanafunzi katika shule za chekechea pia kusimamishwa kwa wiki moja mjini humo.