1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Urusi itaivamia Ukraine

20 Januari 2022

Rais wa Marekani Joe Biden ametabiri kwamba Urusi itaivamia Ukraine akisema itakabiliwa na adhabu kali kwa kuivamia kikamilifu.

https://p.dw.com/p/45oo0
USA Washington | Pressekonferenz Präsident Joe Biden nach einem Jahr im Amt
Picha: Mandel Ngan/AFP

Biden ameyasema haya katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington wakati ambapo waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken akiwa amewasili nchini Ujerumani, kuendeleza juhudi za kutafuta suluhu katika mzozo huo wa Urusi na Ukraine.

Matamshi haya ya Biden yamezua hali ya kutoeleweka jinsi nchi za Magharibi zitakavyojibu iwapo Rais Vladimir Putin atatoa agizo la kuvamiwa kwa Ukraine, jambo lililopelekea ikulu ya White House baadae iweke wazi kuhusiana na kile alichomaanisha Biden.

Marekani imeweka tayari vikwazo na adhabu kwa Urusi

Biden amesema mkutano wa tatu wa kilele na Putin bado unaweza kufanyika baada ya viongozi hao wawili kukutana mara mbili mwaka jana. Amesema ana wasiwasi kwamba madhara ya mzozo wa Ukraine yanaweza kuwa mapana na yasiweze tena kudhibitiwa.

USA Russland Biden und Putin
Rais Joe Biden (kushoto) na Rais Vladimir Putin (kulia)Picha: ERIC BARADAT/AFP

"Na kinachonitia wasiwasi ni kwamba mambo yanaweza kupindukia kwa urahisi sana kwasababu ya yale uliyoyasema, mipaka ya Ukraine na kile ambacho Urusi inaweza au haiwezi kufanya. Natumai kwamba Putin anaelewa kuwa hawezi vita kamili vya nyuklia. Hayuko aktika nafasi nzuri kuitawala dunia," alisema Biden.

Biden na kikosi chake wametayarisha vikwazo na adhabu zengine za kiuchumi kwa Urusi, iwapo itaivamia Ukraine na rais huyo wa Marekani amesema kampuni za Urusi huenda zisiweze kutumia dola ya Marekani tena.

Hayo yakiarifiwa, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken aliwasili mjini Berlin Alhamis kwa mazungumzo ya kidplomasia na marafiki wa Marekani kwa ajili ya kupunguza mvutano ulioko kati ya Urusi na Ukraine.

Anthony Blinken kukutana na Lavrov

Blinken ambaye hapo Jumatano mjini Kyiev aliahidi kwamba Marekani itafuata njia ya diplomasia katika mzozo huo, atafanya mazungumzo na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kabla kuelekea Geneva hapo kesho kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Russland Soldaten der Luftlandetruppen auf Weg nach Kasachstan
Wanajeshi wa UrusiPicha: Russian Defence Ministry/Tass/imago images

Hapu Jumanne, Ujerumani ilidokeza kwamba huenda ikasitisha mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2 unaotokea Urusi iwapo nchi hiyo itaivamia Ukraine.

Urusi nayo imevipeleka vikosi vyake vya majeshi nchini Belarus kwa kile inachokiita mazoezi ya pamoja ya kijeshi na hilo linaipa nafasi ya kuivamia Ukraine kutoka kaskazini, mashariki na kusini.

Miaka nane iliyopita, Urusi ililiteka eneo la Crimea nchini Ukraine na ikawaunga mkono wapiganaji waliokuwa wanataka kujitenga waliokuwa wanadhibiti sehemu kubwa ya Ukraine mashariki ila kwa sasa imekataa katakata nia ya kufanya uvamizi.

Chanzo/Reuters