1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Xi wakutana kurekebisha mahusiano

Bruce Amani
16 Novemba 2021

Rais Joe Biden wa Marekani amemushinikiza mwenzake wa China Xi Jinping kuhusu rekodi ya haki za binaadamu ya Beijing, katika mazungumzo ya video. Xi alionya kuwa China itajibu uchokozi wowote utakaofanywa kuhusu Taiwan

https://p.dw.com/p/433NF
USA I Virtuelles Treffen Joe Biden und Xi Jinping
Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Mazungumzo hayo ya video yaliyofuatiliwa kwa karibu kati ya viongozi wa madola mawili makubwa kabisa duniani yalielezewa na pande zote kuwa ya wazi na ya moja kwa moja wakati pande zote zikijaribu kupunguza joto na kuepusha mzozo. Biden alimkumbusha Xi kuhusu jukumu lao. "Inaonekana kwangu kuwa jukumu letu kama marais wa China na Marekani ni kuhakikisha kuwa ushindani wetu baina ya nchi zetu hautumbukii katika mgogoro, iwe ni kwa kukusudia ama la."

Soma zaidi: Taiwan lazima iwe tayari kujilinda

Ikulu ya Marekani iliyaweka chini matarajio ya mkutano huo, na hakuna tangazo lolote kubwa au hata taarifa ya pamoja iliyotolewa. Lakini, maafisa wa White House walisema viongozi hao wawili walikuwa na mazungumzo mazuri. Xi alimsalimu rais wa Marekani akisema ni Rafiki yake mkubwa na akaunga mkono hisia za Biden katika kauli zake za ufunguzi. "China na Marekani zinapaswa kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani, na kuwa na ushirikiano wa faida kwa pande zote. Ningependa kufanya kazi na mheshimiwa Rais ili kupata maelewano na kuchukua hatua za dhati za kuleta maendeleo ya chanya ya mahusiano ya China na Marekani."

Taiwans Militär
Msafara wa jeshi la Taiwan baada ya China kutishia kuungana na kisiwa hichoPicha: Chiang Ying-ying/AP Photo/picture alliance

Rais Xi ameahidi kutengeneza soko kubwa na fursa  zaidi za maendeleo kwa nchi nyingine. White imesema Biden kwa mara nyingine alielezea wasiwasi kuhusu rekodi ya haki za binaadamu ya China, na kuweka wazi kuwa anataka kuwalinda wafanyakazi wa Kimarekani na viwanda dhidi ya taratibu za China za kibiashara na kiuchumi zisizo za haki.

Walijadili pia changamoto muhimu za kikanda, ikiwemo Korea Kaskazini, Afghanistan na Iran. Biden angetaka kukutana na Xi ana kwa ana, lakini kiongozi huyo wa China hajaondoka nchini mwake tangu kuanza kwa janga la corona.

Soma zaidi: Biden na Xi wahimiza mahusiano thabiti ya Marekani na China

Tofauti kubwa bado zipi kuhusu Taiwan, na ilikuwa wazi baada ya mazungumzo hayo. Ikulu ya White House imesema wakati Biden alisisitiza uungwaji mkono wa muda mrefu wa Marekani wa sera ya China Moja, ambapo inaitambua rasmi Beijing badala ya Taipei, pia alisema kuwa anapinga vikali juhudi za upande mmoja za kubadilisha hali ilivyo au kuhujumu amani na utulivu katika mlango wa bahari wa Taiwan.

Kwa mujibu wa shirika la habari la China Xhinhua, Xi amesema wale walioko Taiwan wanaotafuta uhuru, na waungaji mkono wao nchini Marekani, wanacheza na moto. Xi anapinga juhudi za Washington za kuiweka Taiwan katika mfumo wa kimataifa, na matamshi ya karibuni ya Biden kuwa Marekani itailinda Taiwan katika matukio Fulani pia yalizusha mvutano. China inadai kuwa kisiwa hicho kinachojitawala ni himaya yake. Beijing imeapa kukiweka kisiwa hicho cini ya uthibiti wa China, kwa kutumia nguvu kama itahitajika.

AFP/Reuters