1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Binti Gaddafi amtetea baba yake

Halima Nyanza15 Aprili 2011

Binti wa kiongozi wa Libya, Aisha Gaddafi amesema muungano wa kijeshi wa nchi za magharibi unaotaka baba yake aondoke madarakani ni kuwatukana wa Libya wote.

https://p.dw.com/p/10u0m
Muammar GaddafiPicha: AP

Akitoa hotuba yake mjini Tripoli, katika maadhimisho ya miaka 25, ya Libya kushambuliwa kwa mabomu, wakati Marekani ilipofanya mashambulio ya anga katika mji huo mkuu mwaka 1986, Aisha Gaddafi amesema watoto kadhaa waliuawa wakati huo na sasa baada ya miaka kadhaa mashambulio kama hayo tena yanafanywa kwao na watoto wao.


Huku akishangiliwa na wafuasi wa baba yake katika viwanja vya Bab al Aziziyah, Aisha alisema wanajeshi hao wanataka kumuua baba yake, wakijifanya kuwalinda raia.

Katika taarifa yao ya pamoja ambayo imechapishwa leo, Rais Barack Obama wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, wamesema kumuacha Gaddafi aendelee kuiongoza Libya kutakuwa ni usaliti wa kupita kiasi.

Wakati huo huo, majeshi ya Libya yanadaiwa kuwaua watu wanane baada ya kushambulia kwa roketi mji wa Misrata.

Kwa mujibu wa daktari katika eneo hilo watu wengine saba akiwemo mtoto na mzee walijeruhiwa katika mashambulio hayo.

Wakaazi wa eneo hilo walikiambia kutuo cha teklevisheni cha al Jazeera kwamba takriban roketi 120 zilivurumishwa katika mji huo leo asubuhi.

Katika hatua nyingine, mtandao wa kigaidi wa al Qaeda umeyataka majeshi ya nchi za kiarabu kuingilia kati mzozo wa kisiasa nchini Libya na kumuondoa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Muammar Ghadafi.

Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia mkanda wa video,  kiongozi nambari mbili wa al Qaeda Ayman al Zawahiri, ameyatolea wito majeshi ya nchi za kiarabu kumuondoa kanali Gaddafi, ili hatua ya kuingilia kati kusaidia waasi inayofanywa na majeshi ya nchi za magharibi isije kuwa uvamizi.

Msaidizi huyo wa Osama bin Laden amepongeza pia kuangushwa kwa aliyekuwa rais wa Misri Hosni Mubarak.

Al Zawahiri, ambaye ni Mmisri alikuwa ni mpinzani mkubwa wa utawala wa nchini mwake na kwamba alishawahi kutumikia kifungo gerezani kwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Anwar Sadat katika miaka ya 80.

Wakati mapigano yakizidi kuendelea nchini humo, Malawi imekata uhusiano wake wa muda mrefu wa kibalozi na Libya kutokana na mzozo huo wa kisiasa unaoendelea na idadi kubwa ya raia wanaouawa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya Nchi za nje ya nchi hiyo imesema Malawi itabadili msimamo wake kuhusiana na uhusiano wao baada ya hali kuimarika na maisha kurudi katika hali yake ya kawaida.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Josephat Charo