1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blacksburg Virginia, Marekani. 33 wauwawa.

17 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC9K

Shambulio la risasi katika viunga vya chuo kikuu katika jimbo la Marekani la Virginia limesababisha watu 33 kuuwawa , ikiwa ni pamoja na mtu anayeshukiwa kuwa ni mshambuliaji, ambae polisi wanasema alijiua mwenyewe kwa kujipiga risasi.

Kulikuwa na matukio mawili katika muda wa saa mbili, katika bweni la wanafunzi ambako watu wawili waliuwawa na katika jengo la uhandisi ambako watu 30 wameuwawa pamoja na mshambuliaji.

Maafisa wamesema kuwa wanajaribu kutafuta iwapo matukio hayo yanahusiana na bado hawajamtambua mtu aliyefanya tukio hilo.

Watu 15 wamejeruhiwa. Baada ya tukio hilo baya kabisa katika historia ya Marekani la kushambulia kwa risasi , rais George W. Bush amesema kuwa Marekani imeshtushwa na kuchukizwa.

Chuo hicho kikuu cha taifa katika mji wa Blacksburg, kiasi cha kilometa 400 kusini magharibi ya Washington DC, kina wanafunzi 26,000.

Mauaji hayo katika chuo hicho cha ufundi cha Virginia yanakuwa mabaya zaidi katika viunga vya vyuo vikuu nchini Marekani tangu mauaji yaliyofanyika katika chuo kikuu cha Texas mwaka 1966.