1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter awashambulia wakosoaji wa FIFA

10 Juni 2014

Viongozi wa soka ulimwenguni wanakutana mjini Sao Paulo -Brazil wakati kukiwa na hofu kuhusiana na kitisho cha mgomo wa wafanyakazi wa treni za chini ya ardhi kuvuruga sherehe za Kombe la Dunia

https://p.dw.com/p/1CFGq
Sepp Blatter Sao Paulo
Picha: NELSON ALMEIDA/AFP/Getty Images

Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA linaandaa Mkutano wake mkuu wa 64 wakati kukiwa na wingu kubwa la kashfa ya ufisadi kuhusiana na Qatar kupewa kibali cha kuandaa Kombe la Dunia mwaka wa 2022, kashfa ambayo imezusha shutuma kutoka kwa baadhi ya wafadhili wakuu wa dimba hilo.

Kampuni za Hyundai, Coca Cola, Adidas, Sony na Visa, zinadai uchunguzi ufanywe kikamilifu kuhusiana na madai hayo. Akizungumzia madai hayo Rais wa FIFA Sepp Blatter aliwashambulia wakosoaji akisema wanajaribu “kuharibu” FIFA. Akizungumza kabla ya kuanza mkutano huo, Blatter mwenye umri wa miaka 78 alisema wanaoeneza madai hayo ya ufisadi wana lengo la kuharibu siyo mchezo, bali taasisi ya FIFA kwa sababu ni taasisi imara. Katika matamshi mengine, kiongozi huyo wa FIFA amesema wakosoaji wa Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar wanasukumwa na “ubaguzi wa rangi”.

Mkutano huo unaandaliwa Sao Paulo, mji ambao kwa sasa unakabiliwa na changamoto zake baada ya wafanyakazi wa treni za chini ya ardhi kutishia kuendelea na mgomo wao siku ya Alhamisi, wakati ambapo macho ya ulimwengu mzima yataugeukia mji huo mkubwa wa Brazil kwa ufunguzi wa Kombe la Dunia. Wahudumu hao wanataka nyongeza ya asilimia 12.2 ya mishara yao na kwa sasa mwajiri wao anapendekeza asilimia 8. Huyu hapa mmoja wa wafanayakazi

Symbolbild WM Katar 2022
Wafadhili wa Kombe la Dunia wanadai uchunguzi ufanywe kuhusiana na madai ya hongoPicha: picture-alliance/dpa

Wafanyakazi hao walipiga kura jana kusitisha mgomo wao uliodumu siku tano, na ambao ulisababisha foleni kubwa za magari na kuathiri usafiri kuelekea katika Corinthians Arena, uwanja utakaokuwa mwenyeji wa shereze za ufunguzi pamoja na mechi ya kwanza. Mahakama ilithishia kuwatoza faini wafanyakazi wanaogoma lakini chama chao hakitishiki wala serikali ya mji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na viongozi 12 wa nchi na serikali watakuwa katika uwanja huo, ambao wafanyakazi wanapambana usiku kucha kuumaliza kwa wakati unaofaa.

Lakini kabla ya kuziona timu zao zikimenyana viwanjani, mashabiki wanaowasili nchini Brazil kwanza watalazimika kupambana na mparaganyiko katika viwanja vya ndege, pamoja na foleni za taxi za hadi saa mbili. Viwanja vya ndege vinajiandaa kuwakaribisha mamilioni ya wasafiri wa kimataifa wanaotua nchini humo kwa ajili ya tamasha hilo kubwa la soka. Maafisa wa Brazil wanasisitiza kuwa watakuwa tayari, lakini abiria huenda wakajikuta katika hali ngumu.

Hayo yanajiri wakati timu za mwisho zikiendelea kumiminika nchini humo ambapo vikosi vya Ubelgiji na Nigeria vinatarajiwa kuwasili hii leo. Baada ya hao kuwasili, zitasalia timu tatu pekee kati ya 32 ambazo bado hazijafika: Korea Kusini, Ghana na Ureno. Zote zinatarajiwa kuwa nchini humo hapo kesho.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman