1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter kuiongoza FIFA kwa miaka mingine minne!

2 Juni 2011

Kitakuwa kipindi cha changamoto nyingi huku Blatter akiahidi kufanya mageuzi makubwa kuhusu jinsi FIFA inavyoendesha shuhguli zake.

https://p.dw.com/p/11Ss8
Rais wa FIFA, Joseph Sepp BlatterPicha: ap

Rais wa shirikisho la kandanda ulimwenguni, FIFA, Sepp Blatter, anatakiwa kuwajibishwa kufanya mageuzi huku shirikisho hilo likikabiliwa na kashfa nzito ya rushwa. Hayo yamesemwa na waziri wa michezo wa Australia, Mark Arbib, hapo jana. (01.06.2011) Kwenye mahojiano yake na redio ya ABC jana, waziri Arbib alisisitiza kuwa mageuzi ni muhimu sana wakati huu ndani ya FIFA.

Blatter alichaguliwa tena jana kuiongoza FIFA kwa muhula wa nne. Blatter mwenye umri wa miaka 75, alishinda kura 186 kati ya 203 zilizopigwa, na baada ya hapo kutumia hotuba aliyopaswa kutoa ya ushindi wa uchaguzi huo, kupendekeza mabadiliko katika FIFA.

Waziri mkuu wa Urusi, Vladamir Putin, amempongeza Blatter kwa ushindi wake huo. Putin, ambaye anaonekana kuwa mpambe wa karibu wa Blatter, aliongoza juhudi za Urusi kushinda na kuchaguliwa kuwa muandaaji wa michuano ya kombe la dunia la kandanda mwaka 2018 na kwa mshangao mkubwa kuishinda England.

Blatter alikuwa mgombea pekee baada ya mpinzani wake, Mohammed bin Hammam, kujitoa katika kinyang'anyiro cha kuwania urais wa FIFA mwishoni mwa juma lililopita. Hammam amehusishwa kwenye kashfa hiyo inayohusu uteuzi wa Qatar kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2022. Uingereza hapo awali ililiomba shirikisho hilo kuahirisha uchaguzi huo, baada ya kufichuka wiki iliyopita kuwa Blatter mwenyewe anafanyiwa uchunguzi kufuatia tuhuma zilizomkabili za rushwa.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Saumu Mwasimba