1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boateng asema ataondoka tena uwanjani

5 Januari 2013

Mshambuliaji wa klabu ya Italia AC Milan Kevin-Prince Boateng ameapa kuondoka uwanjani tena kama atakabiliwa na vitendo vya ubaguzi wa rangi bila kujali umuhimu wa mchuano huo.

https://p.dw.com/p/17Edr
AC Milan Ghana midfielder Kevin-Prince Boateng, right, is flanked by his teammate Mathieu Flamini as he gestures towards the crowd in Busto Arsizio, near Milan, Italy, Thursday, Jan. 3, 2012. A friendly match between AC Milan and lower division club Pro Patria was abandoned Thursday after racist chants directed at Milan's black players, the latest incident of racial abuse that continues to blight the sport. After repeated chants directed his way, Ghana midfielder Kevin-Prince Boateng picked up the ball and kicked it at a section of the crowd in the 26th minute of the first half. Boateng then took off his shirt and walked off the pitch with his Milan teammates. Urby Emanuelson, Sulley Muntari and M'Baye Niang were also targeted by the chants. (Foto:Emilio Andreoli/AP/dapd)
Freundschaftspiel AC Mailand gegen Pro Patria Reaktion Boateng rassistische ÄußerungenPicha: AP

Boateng alikabiliwa na matamshi ya kibaguzi kutoka kwa mashabiki wa klabu ya Pro Patria wakati wa mchuano wa kirafiriki siku ya Alhamisi iliyopita, na mshambuliaji huyo Mghana ambaye mzaliwa wa Ujerumani akajibu kwa kuondoka uwanjani akifuatwa na wachezaji wenzake wa Milan. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameungwa mkono na mmiliki wa Milan Silvio Berlusconi na anasisitiza kwamba matukio ya kibaguzi hayapaswi kukubaliwa kuenea katika viwanja vya michezo. Hatua hiyo ya Boateng ya kupinga ubaguzi, ina maana kuwa yuko tayari kuondoka uwanjani wakati wa mchuano mkubwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, au wa ligi ya Italia Serie A, kama itasaidia kuongeza shinikizo kwa matukio ya kibaguzi. Boateng alikuwa amemlalamikia refariii mara tatu kuhusu ubaguzi katika mechi hiyo ya Pro Patria, na hatimaye akaamua kuchukua hatua yeye mwenyewe baada ya hatua kukosa kuchukuliwa na maafisa wa mechi wakati dhihaka zilipozidi kutoka kwa mashabiki.

Holtby kuhamia Tottenham

Klabu ya Tottenham imekubali kumsaini kiungo wa Ujerumani Lewis Holtby kutoka klabu ya Schalke 04 mwishoni mwa msimu huu. Holtby hivi majuzi alitangaza kwamba ataondoka klabu ya Schalke na Spurs wametangaza kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 atahamia Whiteheart Lane wakati mkataba wake na klabu lhiyo ya Ujerumani utakapokamilika.

Lewis Holtby kuhamia Totteham England mwishoni mwa msimu
Lewis Holtby kuhamia Totteham England mwishoni mwa msimuPicha: dapd

Kule England, sera ya klabu ya Chelsea katika kipindi cha usajili wa wachezaji wapya cha mwezi wa Januari, inaonekana kutosheleza gharama ya kuwania mataji na kutimiza bidii ya kifedha. Takribani pauni milioni nane tayari zimechangishwa wiki hii kwa kumwachilia Daniel Sturridge aliyejiunga na Liverpool na kumsajili Demba Ba kutoka Newcastle. Wakati huo huo, Chelsea inaonekana kuonyesha kuwa hakuna nafasi ya kumwongeza mkataba kiungo Frank Lampard licha ya mpenzi huyo wa mashabiki kuonyesha uwezo wake wa kufunga magoli hata wakati akiwa na umri wa miaka 34. Nahidha John Terry amekiri kwamba ataumia moyoni kama Lapmard atahama klabu hiyo. Pia klabu ya Westham imemsaini kiungo Joe Cole kutoka Liverpool, na mshambuliaji wa Arsenal Marouane Chamakh amejiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa mkopo hadi mwishoni mwa msimu. Newcastle iliimarisha safu yake ya ulinzi kwa kusajili beki wa kulia Mathieu Debuchy kutoka Lille ya Ufaransa.

Kombe la AFCON

Kiungo wa Ghana Andre Dede Ayew, huenda akakosa dimba hilo la AFCON baada ya kupatwa na jeraha la mguuni wakati akifanya mazoezi na klabu yake ya Marseille nchini Ufaransa. Ijapokuwa kiwango cha tatizo hilo bado hakifahamiki, maafisa wa Ghana wanasisitiza kwamba mchezaji huyo wa tuzo ya mchezaji bora wa BBC mwaka wa 2011, anajiunga na kambi yao ya mazoezi wikendi hii Abu Dhabi.

Kutokuwepo kwa Dede Ayew kutakuwa pigo kubwa kwa Ghana
Kutokuwepo kwa Dede Ayew kutakuwa pigo kubwa kwa GhanaPicha: AP

Ghana wanatarajiwa kuchuana na Misri na Tunisia katika mechi za kujipima nguvu katika Umoja wa Falme za Kiarabu kabla ya kuelekea Port Elizabeth Afrika kusini kwa mechi za kundi B dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali na Niger. Kukosekana kwa Ayew, kutakuwa pigo kubwa kwa Black Stars wa Ghana, wakati wakilisaka Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza tangu walipowazaba wenyeji Libya kwa mikwaju ya penalti mjini Tripoli miaka 31 iliyopita.

Wakati huo huo kocha wa timu ya wenyeji Afrika Kusini Gordon Igesund amesema mashabiki wao hawapaswi kutarajia mengi zaidi katika mechi za kirafiki dhidi ya Norway mjini Cape town Jumanne ijayo na wenzao waliofuzu Algeria mjini Soweto siku nne baadaye. Igesund tayari ameshindwa michuano mitatu ya kirafiki kati ya mechi sita. Kocha huyo anasema bado hajakikusanya kikosi kamili chenye wachezaji dhabiti watakaoshiriki mechi hizo.

Afrika Kusini itafungua dimba mnamo Januari 19 wakati watakapokabiliana na Visiwa vya Cape Verde katika uwanja wa Soccer City wenye uwezo wa kuwa na mashabiki 90,000 mjini soweto. Kwingineko mshambuliaji wa klabu ya Rizespor Uche Kalu amejiondoa katika kikosi cha Nigeria kitakachoshiriki dimba la AFCON. Kalu amekuwa akisumbuliwa na jeraha na ameamua kuondoka katika kambi ya mazoezi ya Super Eagles mjini Faro Ureno. Nigeria wako tayari kumpa nafasi mshambuliaji wa Newcastle Shola Ameobi nafasi ya mwisho kujiunga na kambi yao ya mazoezi. Mkufunzi mkuu Stephen Keshi amemtaja Ameobi katika kikosi cha mwanzo cha Nigeria lakini mchezaji huyo amekataa kujibu simu za mkufunzi huyo tangu mwezi Desemba. Nigeria itamenyana na mabingwa watetezi Zambia, Burkina Faso na Ethiopia katika kundi C nchini Afrika kusini. Rais wa Togo Faure Gnassingbe ameitisha mkutano na nahodha wa timu ya taifa Emmanuel Adebayor kufuatia kukataa kwake kujiunga na kikosi kitakachoshiriki mechi za AFCON kufuatia mgogoro wa marupurupu na shirikisho la soka nchini humo.

Zambia watalenga kutetea taji lao la AFCON nchini Afrika Kusini
Zambia watalenga kutetea taji lao la AFCON nchini Afrika KusiniPicha: picture-alliance/dpa

Adebayor anatarajiwa wakati wowote kuwasili nchini humo kufanya mazungumzo na rais, ambayo yanatarajiwa kubadilisha msiamamo wake. Togo itafungua kazi dhidi ya Cote d'Ivoire katika kundi D, mjini Rusteburg. Katika kikosi cha Mali, Momo Sissoko wa klabu ya Ufaransa ya Paris Saint Germain, anatarajiwa kujiunga na wenzake baada ya miaka mitatu ambapo aliwahi kuichezea timu y ataifa. Kocha Patrice Carteron amekitaja kikosi dhabiti ikiwa ni pamoja na Mahamadou Diarra wa fulham, na kiungo wa zamani wa Barcelona Seydou Keita. Samba Diakite wa Queens Park Rangers pia amejumuishwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri: Mohammed Dahman