1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram yawateka nyara watu 80 Cameroon

19 Januari 2015

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram, wamewateka nyara watu wapatao 80 baada ya kufanya shambulizi katika eneo la kaskazini mwa Cameroon, siku moja baada ya Chad kupeleka wanajeshi wake kupambana na kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1EMWO
Wapiganaji wa Boko Haram
Wapiganaji wa Boko HaramPicha: picture alliance/AP Photo

Afisa mmoja wa polisi wa Cameroon, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa shambulizi hilo limefanyika jana Jumapili, baada ya wapiganaji wa Boko Haram kuvamia vijiji viwili katika wilaya ya Mokolo karibu na mpaka wa Nigeria. Afisa huyo amesema wapiganaji hao walizichoma moto nyumba na kuwateka zaidi ya watu 60, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Kwa mujibu wa afisa huyo wa polisi, watu kadhaa wameuawa katika shambulizi hilo, ingawa hakutaja idadi ya watu waliouawa.

Jeshi la Cameroon lilianzisha operesheni dhidi ya kundi hilo la kigaidi, kutokana na shambulizi hilo. Huo ni utekaji nyara mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na Boko Haram nchini Cameroon. Majeshi ya Chad yaliingia Cameroon siku ya Jumamosi kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kupambana na Boko Haram, kundi la kigaidi kutoka Nigeria, ambalo limewaua maelfu ya watu kaskazini mwa Nigeria katika kipindi cha mwaka uliopita.

Jumatatu iliyopita, jeshi la Cameroon lilifanikiwa kuwaua wapiganaji 143 wa Boko Haram, baada ya kundi hilo kuivamia kambi ya kijeshi iliyoko eneo la kaskazini. Siku ya Jumamosi, Chad iliwapeleka wanajeshi wake nchini Cameroon na Nigeria, pamoja na magari 400 ya kijeshi na helikopta kadhaa za kivita, kwa lengo la kupambana na Boko Haram.

Picha za satelaiti zilizotolewa na mashirika ya haki za binaadamu
Picha za satelaiti zilizotolewa na mashirika ya haki za binaadamuPicha: Amnesty International/DigitalGlobe

Waziri wa Mawasaliano wa Chad, Hassan Sylla Bakari anasema wanapaswa kuwasambaratisha kabisa magaidi barani Afrika. ''Haiwezekani kuona kwamba moja ya nchi jirani Boko Haram wanawaua watoto, wanawake na wazee, wanavamia vijiji. Hilo haliwezekani. Tutapambana, alisema Waziri Bakari.''

Chad yasema itasonga mbele kuelekea kwa waasi

Akizungumza kutoka mji wa Maltam, Cameroon, mkuu wa operesheni hizo za kijeshi kutoka Chad, Kanali Djerou Ibrahim, ameiambia AFP kwamba leo (19.01.2015), watasonga mbele kuyafikia maeneo waliko waasi hao. Nchini Nigeria, wanajeshi wa Chad wanajaribu kuutwaa tena mji muhimu wa Baga ulioko kwenye kingo za Ziwa Chad, ambao unazitenganisha Chad, Nigeria, Niger na Cameroon.

Mji huo uliangukia mikononi mwa waasi wa Boko Haram mwanzoni mwa mwezi huu. Imeelezwa kuwa uasi mkubwa uliofanywa katika mji wa Baga, huenda ndiyo mbaya zaidi kuwahi kufanywa na Boko Haram.

Wiki iliyoipita, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch, yalichapisha picha za satelaiti zinazoonyesha uharibifu mkubwa uliofanywa katika majengo 3,700 kwenye mji wa Baga, huku mji jirani wa Doron Baga ukiwa umeharibiwa vibaya.

Shirika la Amnesty International limesema kuwa kiasi raia 2,000 wameuawa, lakini jeshi la Nigeria limekanusha madai hayo na kusema kuwa idadi ya watu waliouawa kwenye mji wa Baga, ni 150.

Mashambulizi ya kikatili, mauwaji, mashambulizi ya kujitoa mhanga na utekaji nyara ambavyo vimekuwa vikifanywa na wapiganaji wa Boko Haram, umesababisha vifo vya kiasi ya watu 13,000 kaskazini mwa Nigeria, huku wengine milioni 1.5 wakiwa hawana makaazi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,AFPE
Mhariri:Josephat Charo