1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bolsonaro akataa ushauri wa nje kuhusu moto wa Amazon

Lilian Mtono
23 Agosti 2019

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amepingana na ushauri unaotolewa na mataifa mbalimbali kufuatia hofu ya msururu wa matukio ya moto kwenye msitu wa Amazon.

https://p.dw.com/p/3OML9
Brasilien Präsident Jair Bolsonaro
Picha: picture-alliance/dpa/E. Peres

Kitisho hicho kinatokana na msitu huo unaotajwa kama "mapafu ya dunia", kuharibiwa na mfululizo wa visa vya moto na kuchochea mjadala mkali kuhusu nani wa kulaumiwa. 

Rais Jair Bolsonaro ameandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba serikali yake imefungua milango ya majadiliano, lakini kwa kuzingatia data halisi na pande zote kuheshimiana.

Rais wa ufaransa Emmanuel Macron aliuita moto huo "janga la kimataifa", huku akitoa mwito kwa wakuu wa mataifa yaliyoinukia kiviwanda duniani, G-7 kufanya kikao cha dharura kujadili janga hilo katika mkutano wao wa kilele unaofanyika Ufaransa, mwishoni mwa wiki hii."

Aliandika, "nyumba yetu inaungua. Kwa kweli, msitu wa Amazon, mapafu yanayozalisha asilimia 20 ya hewa ya Oksijen unateketea."

Bolsonaro alijibu kwa kuandika "Ninajuta kwamba Macron anataka kujiimarisha kisiasa kwa kutumia suala hili la Brazil na mataifa mengine ya Amazonia. Mawazo yake ni ya kikoloni kwa kuyataka mataifa ya G-7 kujadili suala hilo bila ya kushirikisha mataifa mengine ya ukanda huo".

Brasilien Waldbrände
Msitu wa Amazon umeungua takriba mara 73,000 tangu Januari hadi Agosti mwaka huuPicha: Reuters/B. Kelly

Bolsonaro anatoa matamshi hayo wakati Brazil ikiwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira utakaofanyika mjini Salvador, kuelekea mkutano wa kilele nchini Chile, mwezi Disemba.

Jamii ya watu wanaoishi kwenye msitu huo wameeleza kusikitishwa kwao na namna msitu huo unavyoteketezwa. Handech Wakana Mura ni kiongozi wa jamii hiyo, "Tunasikitika kwa sababu msitu huu unateketea kila walati, tunahisi hali ya hewa inabadilika na dunia inauhitaji huu msitu. Tunauhitaji pia na watoto wetu wanauhitaji."

Wataalamu wa mazingira wanasema uharibifu kwenye msitu huo ulioongezeka kwa mara tatu ilipofika mwezi Julai ikilinganishwa na mwaka jana umechangiwa na visa vya moto, hii ikiwa ni kulingana na taasisi ya kitaifa ya utafiti wa masuala ya Angani, INPE.

Brasilien Protest indigener Frauen
Jamii inayoishi kwenye maeneo ya Amazon imekosoa mara kwa mara sera ya serikali kwenye msitu huoPicha: Reuters/A. Coelho

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi wake mkubwa kutokana na moto kwenye msitu huo. Aliandika kwenye twitter, "katika wakati ambapo kuna mzozo mkubwa wa hali ya hewa, hatuwezi kubeba mzigo mwingine wa uharibifu wa chanzo kikuu cha Oksijeni na bayoanuwai. Ni lazima Amazon ilindwe".

Mapema, mkuu wa utumishi wa rais Bolsonaro, Onyx Lorenzoni aliyatuhumu mataifa ya Ulaya kwa kuongezea chumvi changamoto za kimazingira nchini Brazil ili kuvuruga maslahi yake ya kibiashara.

Takwimu rasmi zinaonyesha kumekuwepo na visa 73,000 vya moto nchini Brazil katika kipindi cha miezi minane, ikiwa ni idadi ya juu kabisa tangu mwaka 2013.

Nchi jirani, Peru ambayo pia ina eneo kubwa la Amazon imetangaza kujiandaa kupambana na moto huo unaosambaa kwa kasi kutokea Brazil na Bolivia. Paraguay na Bolivia wanapambana kuutenganisha moto huo ambao umeteketeza eneo kubwa la msitu huo ambao ni chanzo cha mvua.