1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Bolsonaro atishia kuingiza Brazil kwenye mzozo wa kikatiba

Mohammed Khelef
8 Septemba 2021

Maelfu ya wafuasi wa Rais Jair Bolsonaro wa Brazil waliandamana kumuunga mkono kiongozi huyo anayezidisha mashambulizi dhidi ya Mahakama ya Juu, akitishia kuitumbukiza nchi kwenye mzozo mkubwa wa kikatiba.

https://p.dw.com/p/404Cw
Brasilien Brasilia | Unabhängigkeitstag: Pro-Bolsonaro Demonstration: Jair Bolsonaro
Picha: Eraldo Peres/AP/picture alliance

Maelfu kwa maelfu ya wafuasi wa Bolsonaro waliijaza mitaa wakiwa na bendera ya rangi ya kijani, manjano na buluu ya taifa kwenye miji mikubwa ya Brasilia, Sao Paulo, Rio de Janeiro na miji mingine siku ya Jumanne (7 Septemba) wakifanya sala za umma na wakipiga mayowe ya kumuunga mkono kiongozi huyo anayekabiliwa na hatua kali za kisheria.

Kwenye hotuba yake mbele ya wafuasi hao, Bolsonaro alitumia maneno makali kuwaelezea majaji wa mahakama ya juu na mfumo wa uchaguzi.

"Ninawaambieni, uamuzi wowote wa Jaji Alexandre Morares kuanzia sasa, rais wenu hatausikiliza. Uvumilivu wa watu umefikia kikomo. Namtaka Bwana Morares aondoke aendelee na maisha yake. Kwetu, yeye hana tena maana," alisema rais huyo anayepingana na utaratibu wa kikatiba wa kura za kieletroniki.

Bolsonaro aliapa kutokuutambua uamuzi wowote wa Mahakama ya Juu dhidi yake na kwamba angeliendelea kupigania "uhuru wa kisiasa" wa wote wanaokandamizwa na mfumo wa kiutawala na kiuchaguzi.

Brasilien Präsident Jair Bolsonaro in Sao Paulo
Rais Jair Bolsonaro akisalimiana na wafuasi wake mjini Sao Paulo.Picha: Amanda Perobelli/REUTERS

Maandamano makubwa zaidi yalishuhudiwa kwenye mji wa Sao Paulo, ambako wafuasi wa Bolsonaro waliugeuza uwanja wa Avenida Paulista kuwa bahari ya kijani na njano.

Maafisa wa usalama wa mji huo wanakisia kuwa watu 140,000 walijitokeza kumuunga mkono Bolsonaro, huku wapinzani wake kwenye eneo la kilomita chache kutoka hapo wakifikia 15,000.

Mamlaka za afya za mji huo zinasema zimeshampiga faini mara ya saba Bolsonaro kwa kuvunja miongozo ya kuzuwia kusambaa maambukizo ya korona kwa kutovaa barakowa.       

Mfano wa Trump?

Bolsonaro, ambaye umashuhuri wake umeshuka sana, anadhamiria kurejesha hamasa ya wafuasi wake katika wakati ambapo anakabiliwa na ukosoaji mkali kutokana na kuporomoka kwa uchumi na mkururo wa kesi dhidi yake na washirika wake wa karibu. 

Brasilien Sao Paulo | Unabhängigkeitstag: Pro-Bolsonaro Demonstration
Maelfu ya wafuasi wa Bolsonaro mjini Sao Paulo.Picha: MIGUEL SCHINCARIOL/AFP/AFP/Getty Images

Kapteni huyo wa zamani wa jeshi mwenye umri wa miaka 66, na ambaye hafichi mapenzi yake kwa utawala wa kidikteta wa jeshi baina ya mwaka 1964 hadi 1985, anakabiliwa na upinzani mkali wa rais wa zamani anayefuata siasa za mrengo wa kushoto, Luiz Inacio da Silva, kwenye uchaguzi wa tarehe 22 Oktoba. 

Uamuzi wa Bolsonaro kuyaitisha maandamano hayo jana katika Siku ya Uhuru wa taifa hilo la Amerika ya Kusini umeelezewa na wapinzani wake kwamba ulilenga kuchochea hisia kali za kizalendo na kuimarisha vita vyake dhidi ya muhimili wa mahakama, kwa namna ile ile ambayo shujaa wake, Donald Trump, aliyekuwa rais wa Marekani, alihamasisha uasi wa Januari 6 dhidi ya bunge la Marekani, kuzuwia kutangazwa Joe Biden kuwa rais.

Wachambuzi wanahofia Bolsonaro atatumia njia ile ile aliyotumia Trump kuutilia mashaka uhalali wa uchaguzi huo endapo atashiriki na kushindwa.