1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouteflika ajiuzulu

Lilian Mtono
3 Aprili 2019

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika amejiuzulu baada ya miaka 20 ya utawala wake pamoja kutokana na maandamano makubwa yaliyodumu kwa wiki sita, yaliyolenga kumshinikiza kiongozi huyo kuondoka.

https://p.dw.com/p/3G7mT
Algerien Präsident Abdelaziz Bouteflika
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Djarboub

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amejiuzulu Usiku wa jana (Jumanne 2 Aprili baada ya miaka 20 ya utawala wake pamoja na maandamano makubwa yaliyodumu kwa wiki sita, yaliyolenga kumshinikiza kiongozi huyo pamoja na washirika wake wa karibu kuachia madaraka.

Tangazo hilo la kujiuzulu limekuja siku chache baada ya mwito kutoka kwa mkuu wa jeshi na mwenye ushawishi mkubwa nchini humo la kumtaka Bouteflika ama kuachia madaraka au kutangazwa kikatiba kuwa hana uwezo tena wa kuongoza kutokana na udhaifu wa kiafya.

Shamrashamra zilionekana kwenye maeneo mbalimbali ya mji mkuu, Algiers, baada ya tangazo hilo huku polisi waliokuwa pembeni wakiwaangalia raia hao.

Baraza la katiba linatarajiwa kukutana kutangaza rasmi hatua hiyo.

Kulingana na katiba, spika wa bunge anachukua madaraka kama rais wa mpito na baada ya siku 90 uchaguzi wa urais utaitishwa.

Abdelkader Bensalah ndiye rais wa sasa wa bunge la Algeria, na mshirika wa karibu wa Bouteflika.

Bado haijawa wazi iwapo hatua hiyo itatuliza hali ya mambo nchini humo, na hususan waandamanaji ambao pamoja na kumshinikiza Bouteflika kuachia ngazi, wanataka kufanyika kwa mageuzi katika mfumo mzima wa utawala unaohusisha washirika wake wa karibu.