1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil: Bolsonaro kupeleka jeshi kuzima moto Amazon

Lilian Mtono
24 Agosti 2019

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro ameahidi kutuma majeshi kukabiliana na moto mkubwa unaoteketeza eneo la msitu wa Amazon lililopo nchini humo, huku akitupia lawama hali mbaya ya ukame kusababisha janga hilo la asili.

https://p.dw.com/p/3OPap
Zypern| Proteste zum Schutz des brennenden Waldes am Amazonas
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Karadjias

Bolsonaro amesema serikali ilikuwa inajua kabisa kuhusu hali ilivyo na itakabiliana na kile alichokitaja "uhalifu wa kimazingira" sawa na namna ambavyo hukabiliana na uhalifu mwingine wa kawaida. 

Brasilien Präsident Jair Bolsonaro
Rais Jair Bolsonaro, amekabiliwa na ukosoaji mkubwa hasa kutokana na sera zake kuelekea msitu huo wa AmazonPicha: Reuters/A. Machado

Rais huyo wa 38 wa Brazil ameyasema hayo wakati alipolihutubia taifa. Amesema kuenea kwa "taarifa za uwongo" zinazohusiana na hali ilivyo kwenye msitu huo wa Amazon "hakutawezesha kamwe kupatikana kwa suluhu".

Viongozi wa dunia watoa neno.

Matamshi hayo ya Bolsonaro yanafuatia ukosoaji mkubwa wa kimataifa kutokana na kushindwa kwake kuulinda msitu huo wa Amazon ambao ni chanzo kikubwa cha mvua na ambao umepewa jina "mapafu ya dunia" kutokana na umuhimu wake huo.

Siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa 7 tajiri zaidi duniani, G-7 huko Ufaransa, viongozi wa mataifa hayo wamekubaliana kwamba mzozo huo wa kimazingira unatakiwa kupewa kipaumbele miongoni mwa ajenda za mkutano huo, na uchunguzi dhidi ya serikali ya Bolsonaro nao ukiongezeka.

Ujerumani, Ufaransa na Ireland jana Ijumaa zilitishia kuachana na mkataba wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya Amerika ya Kusini ya Brazil, Argentina, Paraguay, Uruguay na Venezuela ambayo kwa pamoja yanaunda kundi la Mercosur, hasa kutokana na sera za Brazil kuelekea msitu huo.

Leo Varadkar wa Ireland alilielezea jaribio la Bolsonaro la kuyalaumu mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusika na matukio hayo ya moto kuwa "lililenga kuleta mvurugano."  

Wakati huohuo, rais Donald Trump wa Marekani amesema nchi yake imekwishajiandaa kuisaidia Brazil iwapo itahitaji msaada. Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twotter baada ya kufanya mazungumzo na mwenzake huyo wa Brazil. "kama Marekani inaweza kusaidia kukabiliana na visa vya moto kwenye msitu wa Amazon, tuko tayari kusaidia".