1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil kukata tikiti awamu ya mtoano

23 Juni 2014

Awamu ya makundi katika kombe la dunia inaingia katika kipindi cha kufa kupona leo,(23.06.2014)wakati Brazil inakibarua kuweza kufuzu katika awamu ya mtoano wakati Uholanzi na Chile zinawania nafasi ya kwanza kundi B.

https://p.dw.com/p/1COYw
FIFA Fußball WM 2014 Brasilien Mexiko
Brazil ilipopambana na MexicoPicha: Odd Andersen/AFP/Getty Images

Michezo wa awamu ya makundi inafikia hatua ya kufa kupona kuanzia leo ambapo kundi A litakamilisha michezo yake wakati wenyeji wa kombe la dunia Brazil watakapotiana kifuani na Cameroon mjini Brasilia, wakati huo huo kukiwa na mtanange mwingine mjini Recife kati ya Croatia na Mexico.

WM 2014 Gruppe A 2. Spieltag Kamerun Kroatien
Croatia imewaangusha Cameroon katika mchezo wa makundiPicha: Reuters

Pambano la Croatia na Mexico ndio litakalokuwa na mvuto mkubwa kutokana na ukweli kwamba timu itakayoshinda pambano hilo ndio itakayofanikiwa kuingia katika awamu ya mtoano, iwapo Brazil itatoka kidedea katika mchezo wake na Cameroon. Lakini pia iwapo mchezo huo kati ya Croatia na Mexico utatoka sare, Mexico itakuwa imejihakikishia nafasi katika awamu ya mtoano kwa kuwa hadi sasa ina points 4 kibindoni, wakati Croatia ina points 3.

Uholanzi na Chile kuwania nafasi ya kwanza

Wakati michezo hiyo itakuwa ni awamu ya pili ya michezo ya leo, awali kutakuwa na mapambano katika kundi B, ambapo Australia, Soccerroos, wataingia uwanjani kuminyana na mabingwa wa zamani Uhispania na wakati huo huo Uholanzi ikiwania na Chile nafasi ya uongozi katika kundi lao. Timu hizo zote mbili zimekwisha kata tikiti ya kuingia duru ya mtoano.

Wenyeji Brazil pamoja na kuwa na nyota wao Neymar , pamoja na wachezaji wengine wenye uwezo mkubwa lakini wamekuwa wakihangaika kufikia kiwango chao cha juu cha mchezo.

Ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Croatia na sare ya bila kufungana na Mexico imewaacha wakihitaji point nyingine ya ziada kujihakikishia kusonga mbele. Iwapo Mexico itaishinda Croatia , kikosi hicho cha Luis Felipe Scolari kinaweza hata kukubali kufungwa na Cameroon, licha ya kuwa kipigo hakitaleta taswira nzuri kwa kikosi hicho cha Selecao.

WM 2014 Gruppe G 2. Spieltag Deutschland Ghana
Klose akipachika bao la kusawazisha baina ya Ujerumani na GhanaPicha: Getty Images

Die Manschaft yatikiswa

Kikosi cha Ujerumani kimetikiswa, lakini hakiyumbi sana. Die Mannschaft , kinachoongozwa na kocha Joachim Loew kilipata sare ya jasho ya mabao 2-2 dhidi ya Ghana siku ya Jumamosi mjini Fortaleza , na kikosi hicho kinapiga hatua kuelekea awamu ya mtoano , licha ya kuwa tikiti bado haijakatwa rasmi.

Kuwa na uhakika wa kuingia awamu hiyo ya timu 16, Ujerumani inalazimika kesho kupambana kufa kupona mjini Recife dhidi ya Marekani. Kikosi hicho kimeonesha ujasiri wa hali ya juu wa kupambana kutoka kufungwa hadi kurejesha bao na kupata sare kama anavyosema kocha wa Ujerumani Joachim Loew.

"Wachezaji walichoka sana . Kila mmoja aligundua hivyo. Katika kipindi cha kwanza ulikuwa mchezo wa kutumia mbinu. Kulikuwa na nafasi chache za kufunga. Lakini kipindi cha pili hali ilikuwa piga nikupige. Kulikuwa na kasi kubwa katika mpambano huu. Wachezaji walifanya kila linalowezekana, walifanya kila kitu na walitumia nguvu zote."

Pambano lilikuwa gumu na la kuchosha kutokana na hali ya hewa, lakini Ujerumani ilinusurika na ni muhimu kwa kuwa mpambano dhidi ya Marekani utakuwa wa kuvutia, kama anavyosema mchezaji wa kati wa Ujerumani Sami Khedira.

WM 2014 Gruppe G 2. Spieltag Deutschland Ghana
Asamoah akiweka mpira wavuni Ujerumani na GhanaPicha: Emmanuel Dunand/AFP/Getty Images

"Katika dakika zote 90 ilikuwa ni mapambano. Nafikiri kwa upande wa kimbinu hatukuweza kufanya vya kutosha, kama tulivyotaka , na kama tulivyoonesha katika mchezo wa kwanza, ndio sababu mchezo ulikuwa mgumu kwetu. kitu kizuri , ni kwamba baada ya kupata bao la kuongoza na kuwa nyuma tuliweza kupambana na kurejesha bao. Kwa hilo, nadhani mchezo huo ulistahili kuwa sare kwa timu zote."

Ureno inaning'inia kwa ncha ya vidole katika majaaliwa yao ya kuingia katika duru ya mtoano ya timu 16, lakini itaingia kesho katika mchezo wake wa kundi G dhidi ya Ghana ikiwa na hakika kuwa Marekani na Ujerumani hazitacheza kupata sare tu ambayo itawaingiza wote katika awamu ya mtoano.

Ureno iliweka hai matumaini yake finyu ya kuingia katika awamu ya makundi baada ya kupata bao ya dakika za mwisho ambalo liliipa timu hiyo ya kocha Paulo Bento sare muhimu jana jumapili katika uwanja wa Amazonia.

Hakuna urafiki kati ya Marekani na Ujerumani

Lakini wadadisi wa mambo wanakumbusha kombe la dunia mwaka 1982, ambapo katika mchezo wa mwisho wa makundi Ujerumani iliishinda Austria kwa bao 1-0 na timu zote hizo mbili zikaingia katika awamu ya mtoano. Mara hiyo mhanga alikuwa timu ya Algeria ambayo iliishinda Ujerumani katika makundi kwa mabao 2-1.

WM 2014 Gruppe G 2. Spieltag Deutschland Ghana
Kocha wa Die Manschaft , Ujerumani Jogi LoewPicha: picture-alliance/dpa

Ujerumani na Austria zikaamua kutocheza kwa kutoana jasho na Algeria walitumbua macho tu wakiangalia mpira ukipelekwa huku na huko bila umuhimu wowote kwa dakika tisini na Ujerumani ikapata ushindi inaouhitaji na kusonga mbele na kuitupa kando Algeria.

Mara hii ni Ghana na Ureno ambazo zinaweza kupambana kiume lakini hatimaye ni Ujerumani na Marekani zinazohitaji sare tu kuweza kuingia katika awamu ya mtoano ambazo zinaweza kusonga mbele.

Lakini kocha wa Marekani Jurgen Klinsmann ametoa tahadhari kuwa ,na hapa namnukuu , "timu yetu haiko hapa kwa kutafuta sare", akisitisha minong'ono na kuwahakikishia wenye shaka kuhusu mpango wa kupanga matokeo. Klinsmann amesema hakuna simu za kirafiki zilizopigwa na hawajapigiana simu za kuomba urafiki kati yake na kocha wa Ujerumani Jogi Loew.

Lakini lolote linaweza kutokea kati ya sasa na wakati huo, tusubiri tuone.

US-Nationaltrainer Jürgen Klinsmann
Kocha wa US Boys , Jürgen KlinsmannPicha: Getty Images

Mchezaji wa kati wa Cameroon Alex Song amepewa adhabu ya kutocheza michezo mitatu ya kombe la dunia baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Croatia , limesema shirikisho la kandanda dunia FIFA jana. Mchezaji huyo alitolewa nje kwa kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Croatia Mario Mandzukic mgongoni katika nusu ya kwanza ya mchezo wao ambapo Croatia ilitoka na ushindi wa mabao 4-0 mjini Manaus.

Lineker amkosoa Hodgson

Kocha wa Uingereza Roy Hodgson amesema hasikitiki juu ya uteuzi wa kikosi chake katika kombe la dunia licha ya kutolewa na mapema baada ya kushindwa michezo yake miwili dhidi ya Italia na Uruguay.

Mshambuliaji wa zamani wa Uingereza Gary Lineker ameeleza kuwa Hodgson , amekosea kwa kuamua kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao umeshuhudia wachezaji wawili wa timu ya Liverpool Steven Gerrard na Jordan Henderson waliwa pamoja katika eneo la kati, akishauri badala yake kuwa Hodgson angetumia mtindo wa 4-3-3 na kwamba kwa kutumia mfumo wa kwanza wachezaji wa kati walionekana wachache.

Vale do Lobo Algarve Portugal Roy Hodgson Daniel Sturridge
Kocha wa Uingereza Roy Hodgson akitoa ushauri kwa SturridgePicha: Richard Heathcote/Getty Images

Roy Hodgson amekanusha kwamba hakuona kuwa viungo wa timu hiyo walidhibitiwa. Lakini amesema kuwa washambuliaji wa timu nyingine walikuwa mahiri sana katika umaliziaji kuliko wa Uingereza, na walitumia nafasi walizozipata.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ZR

Mhariri: Josephat Charo