1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil yaishinda Korea Kaskazini 2:1 lakini haikutamba.

16 Juni 2010

Leo ni zamu ya mabingwa wa Ulaya Spain na Uswisi: Bafana Bafana na Uruguay.

https://p.dw.com/p/Ns2q
Luis Fabiano wa Brazil dhidi ya Korea Kaskazini.Picha: AP

BAFANA BAFANA

Kombe la dunia 2010 linaendelea leo kwa wenyeji Bafana Bafana -Afrika kusini, siku ya ukumbusho wa machafuko ya Soweto,1976, ikijaribu kuilaza Uruguay, mabingwa mara 2 wa dunia, na kuondoka na pointi 3 ili kuhakikisha yaingia duru ijayo.

Ni siku pia ya kuwaona Waspain,mabingwa wa ulaya, wakicheza na Uswisi. Spain, imekuwa ikipigiwa upatu mno kwamba, ndio timu ya usoni kabisa kutwaa Kombe la dunia mwaka huu na hasa baada ya jana Brazil, kutolewa jasho na Korea ya Kaskazini. Kabla ya mapambano hayo 2, kwanza timu mbili za Amerika kusini: Chile na Hondurus, zitafungua dimba la hii leo huko Nelsprut.

Afrika Kusini, ilioanza kwa sare ya bao 1:1 na Mexico, siku ya ufunguzi wa Kombe hili ijumaa iliopita, inarudi uwanjani ikijua lazima ishinde leo kuweka hayi matumaini i ya kucheza duru ijayo.Katika kundi hili timu zote 4 ziko pointi sawa-Ufaransa,Uruguay,Mexico na Afrika kusini yenyewe. Isitoshe, mpambano wa leo unachezwa katika ile wanayoiita "Siku ya Vijana" - siku ya mapumziko kwa ukumbusho wa machafuko ya Soweto,1976.

Spain,mabingwa wa Ulaya, wanatazamiwa nao kutamba mbele ya Uswisi na kupeleka salamu zao kwa timu nyengine kubwa kama Ujerumani,Brazil na Argentina kuwa huu ni mwaka wao.

BRAZIL NA KOREA KASKAZINI

Ushindi wa taabu wa mabao 2:1 wa mabingwa mara 5 wa dunia-Brazil jana,umepokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa Brazil nyumbani na hata huko Afrika kusini na hasa uamuzi wa kumuacha nje ya kikosi cha Selecao,Ronaldinho: Mashabiki wengi wamlaumu kocha Dunga wakidai Ronaldinho, alistahiki kuwamo ndani ya kikosi hicho.

Ivory Coast na Ureno, ziliteremka uwanjani jana na kuondoka suluhu 0:0 huku majogoo wao 2-Cristiano Ronaldo na Didier Drogba, hakuna alitia bao.

Hatahivyo, nahodha wa Ureno,Ronaldo, ndie aliepata nafasi bora kabisa mnamo dakika ya 11 ya mchezo kutia bao,lakini mkwaju wake uligonga mwamba wa lango la Corte d'Iviore.

Kwavile, sasa Brazil, imeondoka na pointi 3 kwa kuishinda Korea mabao 2:1, Ivory Coast katika mpambano ujao na Brazil, itapaswa kujizatiti barabara zaidi ,kwani, Korea ya kaskazini , imebainisha ni ngome nzito kuitoboa.

Mwandishi: Ramadhan Ali

Mhariri:Josephat Charo