1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Breivik atinga mahakamani Norway

Admin.WagnerD17 Aprili 2012

Kesi dhidi ya mtu aliyekiri kuhusika na mauaji ya watu 77 wengi wao wakiwa wanachama wa tawi la vijana la chama cha wafanyakazi kinachotawala nchini Norway, imeanza kusikilizwa siku ya Jumatatu mjini Oslo.

https://p.dw.com/p/14eXa
Mtuhumia wa mauaji Anders Behring Beirik akiwasili mahakani
Mtuhumia wa mauaji Anders Behring Beirik akiwasili mahakaniPicha: Reuters

Hata hivyo, kijana huyo, Anders Behring Breivik, mwenye umri wa miaka 33, alikataa kutambua uhalali wa mahakama inayosikiliza kesi yake. Breivik alisema hatambui mahakama za Norway kwa kuwa zinapata mamlaka yake kutoka kwa vyama vya kisiasa nchini humo vinavyounga mkono hali ya kuwa na utamaduni mchanganyiko.

Aliongeza kuwa hatambui mamlaka ya jaji Wenche Elisabeth Arntzen anayesikiliza kesi yake  kwa sababu jaji huyo ni rafiki wa dada wa Waziri Mkuu wa zamani wa Norway, na kiongozi wa chama cha wafanyakazi, Gro Harlem Brundtland.

Jaji Wenche Elisabeth Arntzen, anayesikiliza kesi ya Breivik
Jaji Wenche Elisabeth Arntzen, anayesikiliza kesi ya BreivikPicha: AP

Asalimia kinazi
Akiwa amevalia suti nyeusi, Breivik alitabasamu wakati mlinzi akimfungua pingu baada ya kuwasili katika mahakama hiyo iliyohudhuriwa na kiasi ya watu 200 na kusalimia kwa kutumia alama ya kinazi, kabla ya kushikana mikono na waendesha mashataka na maafisa wengine wa mahakama.

Breivik, mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia na anayeuchukia Uislamu atahudhuria mahakamani kwa siku tano mfululizo akitakiwa kueleza kwa nini alilipua bomu katika jiji la Oslo na kuua watu wanane na kisha kuwapiga risasi watu wengine 69, wengi wao wakiwa vijana waliyokuwa wameweka kambi katika kisiwa cha Utoya nje ya jiji la Oslo.

Manusura wa na ndugu wa wahanga wa mauaji wakitembela kambi ya Utoya
Manusura wa na ndugu wa wahanga wa mauaji wakitembela kambi ya UtoyaPicha: dapd

Asisitiza mauaji hayo yalikuwa muhimu kufanyika
Breivik amekiri kufanya mauaji hayo anayodai yalikuwa ni muhimu ili kuilinda Norway kuchukuliwa na waislamu, lakini amekanusha kuwa na hatia. Katika maelezo yake, Breivik amesema alikuwa analenga makao makuu ya serikali mjini Oslo na kambi ya vijana, ambao anawalumu kwa kuruhusu wahamiaji nchini Norway.

Wakili wake pia amesema kuwa hajutii kitendo chake na kwamba hataomba msamaha kwa kile alichokifanya.

Breivik alionekana kama mtu asiyejali kabisa na hakutingishika wakati akisomewa mashataka ya ugaidi na mauaji, ikiwa ni pamoja na maelezo ya jinsi kila mhanga alivyokufa. Suala muhimu linalopaswa kupatiwa ufumbuzi wakati wa wiki kumi za kesi hii ni afya akili ya Breivik, majibu ambayo yatatoa mwelekeo wa aidha kupelekwa gerezani au kupatiwa tiba ya ugonjwa wa akili.

Picha ya Breivik ikionekana kwenye runinga katika chumba walipo waandishi na ndugu wa wahanga
Picha ya Breivik ikionekana kwenye runinga katika chumba walipo waandishi na ndugu wa wahangaPicha: Reuters

Anaweza kufungwa maisha
Endapo atakutwa hana tatizo la akili, Breivik anaweza kuhukumiwa kifungo hadi miaka 21 au kumuwekea utaratibu mwingine ambapo hukumu hiyo itaongezwa kwa muda ambao ataoneka kuwa ni hatari kwa jamii.

Polisi walilazimika kufunga mitaa iliyo karibu na mahakama hiyo ambayo ilijengwa makhsusi kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo ambapo waandishi wa habari, manusura pamoja na ndugu wa wahanga walifuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

Mahakama hiyo iligawanywa kwa vioo imara ili kumtofautisha mshukiwa na waathirika pamoja na ndugu wa wahanga, ambao wengi wao wanahofu kuwa brievik atatumia kesi hii kuendeleza itikadi yake kali ya kisiasa.

Asema mahakama zitumike kuendeleza agenda za itikadi kali
Katika ilani aliyoichapisha kwenye mtandao kabla ya kufanya mashambulizi hayo, Breivik aliandika kuwa wapiganaji wazalendo laazima watumie kesi za mahakani kuendeleza mapambano.

Breivik aliwambia wachunguzi wa kesi yake kuwa yeye ni mpiganaji katika kundi la wanamgambo wanaopigana vita vya dini lakini uchunguzi hawakupata ushahidi wa kuwepo na kundi hilo na kusema kuwa Brievik alifanya mauaji hayo kivyake.

Ili kuonyesha kuwa akili yake ni timamu, Breivik ametaka watu wenye itikadi kali ya mrengo wa kulia na wale wa kiislamu waje kutoa ushahidi katika kesi yake ili kuonyesha kuwa wapo watu wanaounga mkono mawazo yake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\DPAE
Mhariri: Mohamed Khelef.