1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit, bado mtihani kwa Theresa May

Mohammed Abdulrahman
15 Novemba 2018

Waziri wa Uingereza anayehusika na mchakato wa nchi hiyo kujitenga na Umoja wa Ulaya-Brexit, Dominic Raab, na mawaziri wengine wamejiuzulu kwa kusema hawakubaliani na yaliyomo kwenye makubaliano yaliyoafikiwa.

https://p.dw.com/p/38JJr
Theresa May
Picha: picture-alliance/empics

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May leo amekuwa katika harakati za  kuunusuru mswada wa makubaliano ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, baada ya  Waziri wake anayehusika na mchakato huo unaojulikana kama Brexit na mawaziri wengine kujiuzulu. Wote wanayapinga makubaliano hayo wakisema yatainasa  Uingereza  kwa miaka  kadhaa ijayo. 

Mbali ya waziri Dominic Raab anayehusika na  mchakatao wa kujitoa Umoja wa Ulaya-BREXIT, wengine ni waziri wa kazi na malipo ya uzeeni Esther Mcvery , Naibu waziri anayehusika na Ireland kaskazini  Shailesh Vara na  naibu waziri wa Brexit Suella Braverman. 

Hayo yamekuja wakati ambapo mwandishi mkuu wa masuala ya kisiasa wa gazeti la Daily Telegraph akiandika katika mtandao wake wa Twitte kwa kuzinukuu duru  ambazo hazikutaka kutajwa jina, kwamba mbunge mkongwe  Jacob Rees-Mogg anayepinga Uingereza kubakia Umoja wa Ulaya atawasilisha barua ya kutokuwa na Imani na  bibi May.

Duru zinasema kutokana na kujiuzulu waziri Raab, Gavana wa Benki kuu ya Uingereza  Mark Carney  alitoa  wito wakufanyika  kikao cha vigogo wa masuala ya fedha pamoja na benki kubwa za Uingereza, baada ya sarafu ya Pound Sterling kushuka thamani na hisa katika masoko ya fedha kuteremka. Benki kuu mjini London  ilikataa kusema lolote.

Uingereza inatarajiwa kujitoa katika Umoja wa Ulaya  Machi 29 2019
Uingereza inatarajiwa kujitoa katika Umoja wa Ulaya  Machi 29 2019Picha: picture-alliance/D. Kalker

Akilihutubia bunge House of Commons leo, Waziri mkuu Theresa May alisema wamekuwa wakijitayarisha  na hali ya kutopatikana makubaliano na wanaendelea kujitayarisha kwa hilo kwa sababu ametambua kwamba bado wanahatua nyengine ya majadiliano na Baraza la Ulaya, na baada ya makubaliano ya mwisho kupatikana yatapaswa kurudishwa  bungeni.

May akaongeza kwamba chaguo liko wazi: "Uingereza inaweza kujitoa bila ya makubaliano au Waingereza kuungana na kuunga mkono kile alichokiita, makubaliano bora yatakayoweza kujadiliwa.”

Akijibu swali la mbunge mmoja , May amesisitiza:

"Hatutachukuwa chaguo alilosema la kubakia  Umoja wa Ulaya, bali kwa hakika tutajitoa na hilo litatokea tarehe 29 Machi mwa ujao."

Naibu mkuu wa DUP Nigel Dodds, aliliambia bunge angeweza  kurudia orodha ya ahadi lukuki  ambazo waziri mkuu May alizitoa bungeni,  na kwao wao faraghani kuhusu mustakbali wa Ireland Kaskazini katika uhusiano wa baadaye na Umoja wa Ulaya, lakini anahisi itakuwa ni kupoteza wakati, kwa sababu Bibi May ni mkaidi na ni wazi kwamba  hasikilizi la mtu.

Nafasi ya bunge la Uingereza kuidhinisha makubaliano hayo kabla ya nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya  Machi 29 mwaka ujao 2019, inaelekea inazidi kuwa ndogo. Akiungwa mkono na chama cha  DUP cha Ireland Kaskazini , May ana wingi mdogo katika bunge la  vita 650, lakini chama hicho sasa kinasema hakitoyaunga mkono makubaliano yaliofikiwa na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Reuters,AP

Mhariri: Iddi Ssessanga