1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Kansela wa Ujerumani kukutana na Theresa May

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
8 Aprili 2019

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May atafanya mazumgumzo na viongozi wa Ujerumani na Ufaransa kabla ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaojadili Brexit baadae wiki hii.

https://p.dw.com/p/3GTLD
Rede Theresa May zu Brexit-Aufschub
Picha: Getty Images/J. Taylor

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May atakutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin hapo kesho Jumanne na kisha atakwenda Paris kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Katika mazungumzo yake na viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa waziri mkuu wa Uingereza atahitajika kaueleza ni kwa nini ameomba kuongezewa muda hadi tarehe 30 Juni.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watakutana mjini Brussels siku ya Jumatano kujadili ombi la bibi May. Hatua ya kuongezewa muda inahitaji kuidhinishwa na viongozi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jeremy Hunt amesema anataraji kuwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaona kuwa waziri mkuu May anajitahidi kupata suluhisho la Brexit. Amesema waziri Mkuu May anajaribu kila njia kutatua mgogoro huu wa Brexit. Sote tunataka suala hili litatuliwe kwa haraka iwezekanavyo, kwa hiyo sisi, na hivyo tunafanya kila linalowezekana kupata makubaliano kuhusu mchakato wa Brexit . 

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo na Uingereza Michel Barnier
Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo na Uingereza Michel BarnierPicha: Reuters/Y. Herman

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo na Uingereza Michel Barnier amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Ireland, Simon Coveney mjini Dublin kabla ya kukutana na waziri mkuu wa nchi hiyo Leo Varadkar.

Bwana Barnier anafanya mazungumzo hayo nchini Ireland muda wa saa 48 kabla ya May kuanza juhudi za kuwashawishi viongozi wa Umoja wa Ulaya wakubali maombi yake ya kutaka Uingereza iongezewe muda kabla ya kujiondoa Umoja wa Ulaya. Na ikiwa umoja huo utayakataa maombi ya May, Uingereza italazimika kutoka kwenye umoja huo kwa njia ya vurumai na bila ya mkataba Ijumaa ijayo siku iliyopangwa na Umoja wa Ulaya.

Wasiwasi juu ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba ni mkubwa sana katika Jamhuri ya Ireland ambayo ni nchi pekee ya Umoja wa Ulaya yenye mpaka na Uingereza. Taratibu zozote za ukaguzi ama vizingiti vyovyote kwenye mpaka huo vitauathiri sana uchumi wa Ireland na pia kuhujumu mchakato wa amani wa Ireland Kaskazini.

Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wa chama cha Kihafidhina kinachoongozwa na May wanataka kuwasilisha bungeni kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu huyo. Naibu kiongozi wa kundi la chama cha kihafidhina linalounga mkono Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya leo ametoa wito wa kuitisha kura ya kutokuwa na imani na May. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la televisheni la Sky News, naibu kiongozi huyo Mark Francois amesema katika barua aliyomwandikia mwenyekiti wa chama cha Kihafidhina kwamba May anapaswa kujiuzulu. Francois amesema mambo hayawezi kuendelea chini ya kiongozi dhaifu, baraza la mawaziri lililogawika na chini ya chama kilichokata tamaa. Mwanasiasa huyo amesema Theresa May ameshindwa kama kiongozi wa chama ambacho anatishia kukitokomeza.

Vyanzo:/AP/RTRE/AFP