1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit kizungumkuti. Malkia alifungua bunge.

Lilian Mtono
14 Oktoba 2019

Majadiliano ya Brexit yameendelea kukabiliwa na mkwamo hii leo baada ya wanadiplomasia kuashiria kwamba umoja huo ulitaka maridhiano zaidi kutoka kwa waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson.

https://p.dw.com/p/3RGC2
Großbritannien London | Wiedereröffnung des Parlaments - Queen Elizabeth II
Picha: Reuters/T. Akmen

Uingereza inajiandaa kuondoka kutoka Umoja wa Ulaya Oktoba 31 na mkutano wa kilele wa viongozi wa umoja huo unaofanyika Alhamisi hii ama Ijumaa unachukuliwa kama fursa muhimu na ya mwisho ya kuthibitisha makubaliano ya talaka ya Uingereza kutoka kwa Umoja wa Ulaya. Waziri mkuu Boris Johnson anasisitiza taifa hilo litaondoka tu mwishoni mwa mwezi ama kwa makubaliano au hata bila ya makubaliano. 

Pamoja na majadiliano ya pande zote mbili mwishoni mwa wiki ya kupata makubaliano ya dakika za mwisho mwisho, lakini bado pande hizo zinakiri pengo kubwa baina yao.

Msemaji wa Johsnon, James Slack amesema ingawa mazungumzo hayo yalikuwa ya kujenga, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa. Majadiliano hayo yalijikita kwenye vizingiti vinavyohusiana na mustakabali kuhusu mpaka kati ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja huo na Ireland ya Kaskazini, ambayo ni sehemu ya Uingereza. 

Mwanadiplomasia wa Umoja huo mwenye uelewa wa mazungumzo hayo, amesema kuna uwezekano kwamba muda wa Brexit ukasogezwa kwa miezi mitatu, ili kuyabadilisha mapendekezo hayo na kuwa makubaliano yanayofungamana kisheria. 

Lakini waziri wa mambo ya nje wa Ireland Simon Coveney amesema mjini Luxembourg kwamba upo uwezekano wa kupatikana kwa makubaliano, ama mwezi huu au hata wiki hii, huku akionya bado hawajafika huko.

Großbritannien London | Wiedereröffnung des Parlaments - Queen Elizabeth II
Wakosoaji wanasema ajenda hiyo iliyosomwa na Malkia Elizabeth II haitekelezekiPicha: Getty Images/AFP/T. Melville

Jijini London, Malkia Elizabeth II hii leo ameisoma ajenda ya kisheria ya Brexit iliyoandaliwa na serikali ya Johnson, kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa bunge.

Hotuba hiyo ya dakika kumi, iliyosomwa na Malkia Elizabeth mwenye miaka 93, na iliyoandaliwa na serikali ilikuwa na miswada zaidi ya 20, ambayo ni pamoja na sheria ya utekelezwaji wa makubaliano ya Brexit. Alinukuliwa akisema "Serikali yangu itaendelea kuhakikisha raia wa Ulaya ambao wameyajenga maisha yao na wenye mchango mkubwa hapa Uingereza wanapata haki ya kubaki. Muswada huo utajumuisha hatua za kutekeleza ahadi hii. Hatua zitachukuliwa ili kutoa uhakikisho, uthabiti na fursa mpya kwa huduma za kifedha na sekta za kisheria".

Wakosoaji wameitaja hotuba hiyo kuwa isiyotekelezeka, kwa kuwa serikali ya Johnson haina uungwaji mkono mkubwa wa bunge, lakini pia kufuatia uwezekano wa kufanyika uchaguzi miezi michache ijayo, iwapo Uingereza itaondoka ama la ifikapo Oktoba 31.