1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari: Uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Rashid Chilumba15 Februari 2019

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema serikali yake imejizatiti kuhakikisha uchaguzi wa hapo Jumamosi unakuwa wa huru na haki na kuahidi waangalizi wote wa kigeni kwenye uchaguzi huo watakuwa salama. 

https://p.dw.com/p/3DRG8
Nigeria Muhammadu Buhari
Picha: picture alliance/AP Photo/S. Aghaeze

Katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa jana usiku, rais Buhari ambaye anawania kuchaguliwa tena kuiongiza Nigeria kwa miaka minne ijayo, amesema raia wa nchi hiyo wanapaswa kuziweka kando tofauti zote zinazoweza kutishia usalama kuelekea uchaguzi wa Jumamosi na kuwatolea wito vijana kutotumika kama chanzo cha vurugu.

Zaidi ya wapigakura milioni 84 wameandikishwa kushiriki uchaguzi wa jumamosi.

Buhari ameongeza kuwa uchumi wa Nigeria ambao ndio mkubwa kote barani Afrika umeanza kuimarika baada kudorora mwaka 2016 na kutoa ahadi ya kuimarisha zaidi ukuaji wa uchumi na maendeleo pindi atachaguliwa.

Kadhalika rais Buhari amesema serikali yake itatoa ulinzi kamili kwa wanadiplomasia na waangalizi wote wa uchuguzi kutoka nje siku kadhaa baada ya kuandamwa na shinikizo kuhusiana na matamshi yake kuwa mataifa ya kigeni yanalenga kuingilia upigaji kura nchini humo.

Kampeni za lala salama zamalizika

Wahlkampf Nigeria Wahlplakat APC
Picha: DW/T. Mösch

Pazia la kampeni lilifungwa hapo jana ambapo rais Buhari alifanya mkutano wake wa mwisho kwenye jimbo alikozaliwa la Katsina. 

Buhari ambaye ameendesha kampeni yake kwa kuyapigia upatu mafanikio ya utawala wake wa miaka minne aliwarai wapiga kura kutofanya makosa na badala yake wakichague chama chake cha APC ili kuendeleza juhudi za kuimarisha uchumi na kupambana na makundi ya itikadi kali.

Katika sehemu ya hotuba yake rais Buhari alisema "Uharibifu ambao ukosefu wa usalama na rushwa umesababisha katika maisha yetu haupimiki, hata hivyo, inatia moyo kuona mapambanao yetu dhidi ya maovu hayo maiwili yanapata nguvu na kuanza kuleta mafanikio ya wazi."

Kwa upande wake mpinzani mkuu wa rais buhari kwenye uchaguzi huo  Atiku Abubakar  alihitimisha kampeni zake katika eneo alikokulia la Adamawa.

Vor Wahlen in Nigeria  Muhamadu Buhari (M), Präsident von Nigeria, und Atiku Abubakar (r)
Picha: picture-alliance/AP/B. Curtis

Kwenye kile alichokiita kuwa hotuba ya hali ya taifa wakati mkutano wa mwisho wa kampeni, mgombea wa upinzani Atiku Abubakar alisema serikali inayomaliza muda wake imeshindwa kusimamia ulinzi wa taifa, imeendesha kampeni ya upendeleo dhidi ya rushwa na kuudhoofisha uchumi.

Atiku ambaye ni makamu wa rais wa zamani na mgombea wa chama cha Peoples Democratic (PDP) amewataka wapiga kura kutokubali miaka minne mingine ya utawala usio na dira na uongozi usiofaa na kwamba kuchaguliwa tena kwa serikali ya Buhari itakuwa janga kwa Nigeria.

Hofu ya usalama bado ni kikwazo kuelekea uchaguzi

Hata hivyo hofu juu ya usalama imeongezeka baada ya wanamgambo wa Nigeria kutishia  kwamba wataliharibu taifa hilo iwapo Rais Muhammadu Buhari atachaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo.

Kundi la Niger Delta Avengers limefafanua kwamba lina matumaini ya kuubadilisha utawala wa Buhari kupitia uchaguzi na kwamba mtu anayefaa kuiongoza Nigeria ni mgombea wa upinzani, Atiku Abubakar.

Wakati uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa wa utulivu katika historia ya Nigeria, chaguzi za hapo kabla zimekuwa zikiandamwa na vurugu  zinazotokana na tofauti kubwa za kidini na kimaeneo zilizokuwemo nchini humo.

Mwandishi: Rashid Chilumba/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo