1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUJUMBURA: Waandishi watatu waachiliwa huru

4 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCda

Waandishi watatu wa habari nchini Burundi waliokuwa wakizuiliwa kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa baada ya kuripoti kuhusu njama ya kuipindua serikali, wameachiliwa huru.

Mahakama ya mjini Bujumbura imesema hakuna ushahidi kwamba waandishi hao wa redio za kibinafsi walitangaza habari za kutishia usalama wa taifa. Muongozaji mashtaka wa serikali alitaka wahukumiwe kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Matthias Manirakiza, kiongozi wa redio ya Isanganiro alitiwa mbaroni mnamo tarehe 29 Novemba mwaka jana kwa kuidhinisha kutangazwa kwa habari ambazo zingeweza kuhatarisha usalama wa taifa na umma.

Wakili wake, Raphael Gahungu, aliwaambia waandishi wa habari baada ya uamuzi huo wa mahakama kwamba kumekuwa na uvunjaji mkubwa wa sheria na washukiwa walinyimwa haki yao ya kuwa huru.