1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buldoza la Hamas labomoa ukuta mpakani Misri na Gaza

26 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cxve

CAIRO: Maelfu ya Wapalestina kwa mara nyingine tena wamemiminika Misri baada ya wanamgambo wa Hamas kubomoa ukuta na uzio kwenye kivuko cha mpakani cha Rafah,kati ya Misri na Ukanda wa Gaza.Vikosi vya Misri vilishindwa kuzuia umati uliotiririka.Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,tangu siku ya Jumatano kama wakaazi 700,000 wa Gaza wameingia Misri kujinunulia chakula na bidhaa za mahitaji ya kila siku.Juma lililopita,Israel ilifunga njia zote za kuingia na kutoka Gaza na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa bidhaa muhimu katika Gaza.Israel na Marekani zimetoa mwito kwa Misri kufunga kivuko cha mpakani,zikihofia kuwa njia hiyo itatumiwa kupenyeza wanamgambo na silaha.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas wanatazamia kukutana siku ya Jumapili kujadili njia ya kuendelea na mazungumzo ya amani.Wakati huo huo,chama cha Hamas kimekubali mwaliko wa Misri kwenda Cairo kujadiliana na chama cha Fatah cha Rais Abbas.Umoja wa Ulaya umetoa mwito kwa Israel kufungua vivuko vya mpakani vilivyofungwa kufuatia mashambulizi ya makombora yanayorushwa kutoka eneo la Gaza hadi Israel.