1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Cuba kumchagua Kiongozi mpya

Mazula,Scholastica22 Februari 2008

Waziri wa ulinzi wa Cuba Raul Castro anayekaimu nafasi ya Kiongozi wa taifa hilo, anatajwa kuwa na uwezekano wa kuchaguliwa hapo kesho na bunge la taifa kuwa mtu atakayemrithi Fidel Castro aliyetangaza kujiuzulu mapema

https://p.dw.com/p/DBqi
Fidel Castro(Kushoto) na nduguye Raul.Picha: AP

Waziri wa ulinzi wa Cuba Raul Castro anayekaimu nafasi ya Kiongozi wa taifa hilo, anatajwa kuwa na uwezekano wa kuchaguliwa hapo kesho na bunge la taifa kuwa mtu atakayemrithi Fidel Castro aliyetangaza kujiuzulu mapema wiki hii. Lakini pamoja na hayo kuna majina mengine yanayotajwa.Castro ameitawala Cuba kwa karibu miaka 50.

Licha ya Raul Castro mwenye umri wa miaka 76 ana ambaye ni nduguye Fidel Castro kupewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi, pale bunge la taifa litakapokutana kesho, hata hivyo kuna majina mengine yanayotajwa ya kile kinachoitwa "kizazi cha vijana."

Wagombea hao wengine wa uongozi huo wa juu wa taifa hilo la kikoministi ni maafisa wa ngazi ya juu kama Makamu wa rais Carlos Lage mwenye umri wa miaka 56 na Waziri wa mambo ya nchi za nje Felipe Perez Roque ambaye umri wake ni miaka 42.

Pamoja na hayo wadadisi wengi bado wanaashiria ni Raul atakayeibuka mshindi. Baada ya miongo kadhaa ya kuwa waziri wa ulinzi, alitokeza mwaka mmoja na nusu uliopita kukaimu nafasi ya Kaka yake Fidel mwenye umri wa miaka 81, ikielezwa ilikua kwa muda hadi afya ya kiongozi huyo mkongwe itakapo kua nzuri.

Wakati fununu zilipozidi kuhusu haoli ya afya ya Fidel Castro, Raul akatangaza mwezi uliopita kwamba bunge la taifa litamchagua rais mpya wa Cuba Februari 24 na wadadisi kuadhiria huenda asiwe Castro. Kwa hakika hawakukosea kwani wiki iliopita katika barua iliochapishwa katika mtandao wa dola na gazeti la chama cha kikoministi, Fidel Castro akasema hatokua tena mgombea si wa Urais wala kamanda mkuu.

Wachambuzi wanamtaja nduguye Raul kuwa mtu mgumu lakini mwenye kupima hali halisi na ni mpole ukimlinganisha na kaka yake mwenye heba zaidi na msomi, mtu maarufu aliyekua na uwezo wa kuhutubia kwa muda wa masaa manne.

Raul wakati wote amekua nafasi yapili katika ngazi za uongozi wa baraza la taifa na kikatiba alikua anayepaswa kujaza nafasi ya Castro pindi anapokua hayupo, mgonjwa au wakati wa kifo. Na ndivyo ilivyokua akikaimu nafasi hiyo wakati Castro alipojiondoa kwa muda kwa sababu ya ugonjwa hadi alipüoamua kujiuzulu

Wakati wote Raul amekua bega kwa bega na Kaka yake Fidel mwanzoni mwa mapmbano ya kuuangusha utawala wa Batista ulioungwa mkono na Marekani Desemba 1956, hadi yalipofabnikiwa mapinduzi dhidi ya utawala huo 1959.

Hata hivyo wachambuzi wakimarekani na wacuba wanaishi uhamishoni wanasema Raul ni mtu mwenye msimamo mkali kuliko Castro.

Kwa wagombea wengine kama Makamu wa rais Carlos Lage na Waziri wa mambo ya nchi za nje Felipe Perez Roque, wengi wanahisi hawana nafasi mbele ya Raul, licha ya kwamba kunaonekana haja ya kuwepo kwa viongozi vijana ,kwa matumaini ya kupatikana mabadiliko.

Bw Lage ni mmoja kati ya makamu watano wa rais na alitoa mchango mkubwa katika mageuzi ya kiuchumi yaliomsaidia Castro kuepukana na msukosuko mkubwa miaka 1990 kutokana na kuporomoka kwa iliokua Urusi ya zamani ambayo ikiisaidia Cuba kifedha.

Kwa wakati huu Bw Lage pia ni katibu mkuu wa kamati kuu ya baraza la mawaziri akiwa sawa na Waziri mkuu. Anatajwa kuwa ni mtu wa kawaida na hata wakati mmoja ilikua ni kawaida kwake kufika kazini akitumia Baiskeli badala ya gari ya serikali.

Wapinzani wa utawala wa Castro wanasema hawatarajii mabadiliko yoyote chini ya uongozi wa Raul. Pamoja na hayo kuna wenye matumaini kwamba huenda kuondoka madarakani Fidel kutatoa mwanga kuelekea hatima ya Cuba, kiu kikubwa kikiwa ni mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Kwa yeyote atakayechaguliwa hapo kesho, hatua hiyo itamaliza karibu miaka 50 ya utawala wa Fidel Castro na pengine kufungua ukurasa mpya nchini Cuba, wakati Castro akiendelea kukumbukwa na pande zote mbili mahasimu na wafuasi wake.