1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Somalia labatilisha nyongeza ya muhula wa Rais

2 Mei 2021

Wabunge wa Somalia wamepiga kura kwa kauli moja kufuta nyongeza ya miaka miwili kwenye muhula wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed waliyoidhinisha mwezi uliopita baada ya kuzuka mvutano mkubwa kuhusu suala hilo.

https://p.dw.com/p/3sqdh
Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed
Rais Mohammed Abdullahi Mohammed wa Somalia Picha: Vladimir Smirnov/TASS/imago images

Sheria ya kurefusha muda wa utawala wa rais Mohamed ilishuhudia kuzuka makabiliano kati ya pande hasimu za wanajeshi kwenye mkuu wa taifa hilo, Mogadishu, waliogawika juu ya suala hilo.

Zoezi la kura kubatilisha sheria hiyo lilirushwa moja kwa moja na televisheni nchini Somalia na lilifanyika muda mfupi baada ya rais Mohamed kulihutubia bunge na kutangaza nia ya kuitisha uchaguzi wa bunge uliocheleweshwa.

Katika hotuba yake baada ya kura ya bunge, waziri mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble ameamuru wanajeshi kurejea kwenye makambi na wanasiasa kuacha kuchochea vurugu.

Roble pia aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa serikali itafanya mipango ya kuandaa uchaguzi hivi karibuni. Muhula wa rais Mohamed ulimalizika mwezi Februari lakini bila ya kuwepo kwa wabunge wapya, bunge la nchi hiyo lisingeweza kumchagua rais mpya.

Urefushaji muhula wa rais uliwakasirisha wahisani 

Jaribio la rais Mohamed Abdullahi la kurefusha muda wake madarakani pia limewakasirisha wafadhili wa kigeni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiiunga mkono serikali yake kwa matumaini ya kurejesha uthabiti baada ya miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka tangu mwaka 1991.

Somalia Abstimmung Gesetzesentwurf zur Verlängerung der Amtszeit von Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed
Wabunge wa Somalia Picha: Feisal Omar/REUTERS

Nyongeza ya muhula wa rais iliidhinishwa na Baraza la Wawakilishi mwezi uliopita lakini ilipingwa na Baraza la Seneti na kuzusha mzozo wa kisiasa uliozidi makali wiki iliyopita.

Kati ya watu 60,000 hadi 10,000 walilazimika kuzikimbia nyumba zao Jumapili iliyopita baada ya kuzuka mapambano ya silaha kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono rais Mohamed na wale wanaopinga hatua ya kurefushwa kwa muhula wake madarakani.

Mzozo huo wa kisiasa umezidisha wasiwasi kuwa kundi la itikadi kali la Alshabaab linaweza kutumia ombwe la usalama la  ya kuzuka pande hasimu ndani ya jeshi kufanya mashambulizi.

Hatua ya Bunge yakaribishwa kwa bashasha na tahadhari 

Somalia Gewalt zwischen Regierung und Opposition
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Kura ya kufuta nyongeza wa muda imekaribishwa na Marekani, Umoja wa Ulaya na Uturuki ikitajwa kuwa hatua muhimu kuelekea kurejesha hali ya kawaida nchini Somalia.

Marekani imetoa wito kwa pande zote nchini humo kukutana na kukamilisha taratibu za kufanyika uchaguzi wa bunge katika njia ya uwazi na ushirikiano.

Mbunge wa upinzani Abdirahman Odowaa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mengi yanatakiwa kufanywa na kumtaka rais Mohamed kuweka kwa maandishi kile kilichokubaliwa.

"Kukabidhiti mchakato wa ulinzi na uchaguzi kwa waziri mkuu kunapaswa kuwa kwa maandishi na kusainiwe" amesema Odowaa.