1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani kuliidhinisha Jeshi kupambana dhidi ya IS

4 Desemba 2015

Bunge la Ujerumani leo linatarajiwa kuidhinisha kutumwa kwa wanajeshi wa nchi hiyo nchini Syria kupambana dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS.

https://p.dw.com/p/1HHIr
Picha: Reuters/F. Bensch

Iwapo hatua hiyo ya kijeshi itaidhinishwa na bunge, Ujerumani itajiunga na Marekani, Ufaransa na Uingereza katika juhudi kabambe za kuishambulia IS.

Jeshi la Ujerumani linatarajiwa kuimarisha ushirikiano na nchi washirika dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS kwa kutuma ndege sita za kijeshi za kufanya shughuli za upelelezi, ndege ya kujaza ndege nyingine za kijeshi mafuta na manowari ya kuilinda manowari ya Ufaransa ya kubeba ndege za kivita, Charles de Gaule.

Takriban wanajeshi 1,200 pia wanatarajiwa kutumwa Syria. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amesema mashambulizi ya angani na kuwepo kwa majeshi ya ardhini ndio mkakati bora wa kupambana dhidi ya IS.

Wanajeshi kuwepo Syria kwa mwaka mmoja

Von der Leyen hata hivyo amesisitiza hakutakuwa na ushirikiano na majeshi ya serikali ya Rais wa Syria Bashar al Assad. Iwapo hatua hiyo itapitishwa, wanajeshi hao huenda wakatumwa mwezi ujao Syria kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Ndege za kijeshi za Ujerumani
Ndege za kijeshi za UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/B. Wüstneck

Huku hayo yakijiri, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametaka wanajeshi wa ardhini wa Syria na wa nchi za kiarabu kupambana dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu IS ili kundi hilo liweze kushindwa kikamilifu.

Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE waliokuwa wakikutana jana mjini Belgrade, Kerry ameonya mashambulizi ya angani pekee hayawezi kulishinda kundi la IS na kusema kuna haja ya kuwepo kwa wanajeshi wa ardhini wa kutoka nchi za kiarabu kufanikisha kampeini dhidi ya IS.

Matamshi ya Kerry yanakuja baada ya Uingereza kuanzisha mashambulizi ya angani nchini Syria dhidi ya ngome za IS. Ndege za kijeshi za Uingereza zilishambulia visima vya mafuta hapo jana mashariki mwa Syria vinavyowaingizia wanamgambo wa IS fedha zinazowasaidia kutanua uasi wao.

Mashambulizi hayo ya angani yanafuatia uamuzi wa bunge la Uingereza siku ya Jumatano kuidhinisha nchi hiyo kufanya mashambulizi Syria.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema wanapanga kuanzisha mazungumzo kati ya pande zinazozana Syria na kuanzisha kampeini ya kusitisha mapigano kote Syria ifikapo mwezi Januari.

Putin asema Umoja ni nguvu

Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa upande wake ametaka kuwe na juhudi kubwa zaidi za kupambana dhidi ya ya IS. Katika hotuba yake kwa taifa hapo jana, Putin ameishutumu Marekani na washirika wake kwa kuzigeuza Iraq, Syria na Libya kuwa maeneo ya vita na zisizokuwa na utawala huru hali ambayo ni kitisho kwa ulimwengu mzima.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/S. Karpukhin

Putin amesema kila mmoja anapaswa kuacha malumbano na tofauti zilizopo na kufanya juhudi kubwa zaidi dhidi ya ugaidi ambayo itajikita katika misingi ya sheria za kimataifa kuambatana na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Wanadiplomasia waliokuwa wakihudhuria mkutano wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE mjini Belgrade wamesema njia pekee ya kuwa na mkakati bora dhidi ya ugaidi ni kushirikiana.

Mwandishi: Caro Robi/ap

Mhariri: Daniel Gakuba