1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Ujerumani lapitisha muswada wa chuki dhidi ya Wayahudi

Grace Kabogo
19 Januari 2018

Wabunge wa Ujerumani wamepitisha muswada wa kuanzisha sheria kali kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2r8h7
Symbolbild Antisemitismus in Deutschland
Picha: picture alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic, CDU pamoja na chama cha Social Democratic, SPD, chama kinacholinda mazingira cha Kijani na chama kinachowapendelea wafanyabiashara cha Free Democratic, FDP vimepiga kura kuunga mkono kuanzishwa kwa nafasi wa kamishna na kutekeleza mkakati wa kuondoa mizizi ya chuki dhidi ya Wayahudi pamoja na uhalifu kama sehemu ya mapendekezo ya hatua ya 17.

Chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wahamiaji, AfD kimeunga mkono pendekezo hilo, huku chama kinachofuata siasa za mrengo wa kushoto, Die Linke kikijizuia kupiga kura.

Katika hilo, vyama vinasema kuwa uhalifu wa chuki dhidi ya Wayahudi huenda ukaendelea hasa ukihusishwa na vyama vinavyofuata siasa kali za mrengo wa kulia, lakini suala la uhamiaji kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini umelizidi tatizo hilo.

Naibu  kiongozi wa chama cha SPD, Kerstin Griese amesema ilikuwa ni shida sana neno ''Uyahudi'' lilikuwa miongoni mwa maneno ambayo yanatumika sana kwa kutusi katika maeneo ya shule za Ujerumani. Ameongeza kusema kuwa ilikuwa ni muhimu kupinga aina zote za chuki dhidi ya Wayahudi, huku Ujerumani ikichukua jukumu maalum.

Waislamu na AfD

Katika hotuba yake, mwanasiasa wa AfD, Beatrix von Storch amedai kuwa Waislamu wanaoishi Ujerumani walikuwa wakiunga mkono chuki dhidi ya Wayahudi na ametoa wito wa kurejeshwa katika nchi zao, wakiwemo Maimamu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihubiri chuki.

Deutschland Bundestag Debatte zum Thema Antisemitismus | Übersicht
Wabunge wa Ujerumani Picha: imago/C. Ditsch

Matamshi hayo yamekosolewa na Stefan Ruppert wa FDP, ambaye amesema kwamba Von Storch alikuwa akipuuza tatizo lililoko ndani ya chama chake mwenyewe.

Kiongozi wa wabunge wa chama cha CDU, Volker Kauder, katika mahojiano kwenye kipindi cha televisheni cha Morgenmagazin cha hapa Ujerumani, amesema Ujerumani lazima ichukue hatua madhubuti kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi kwani hilo ni jambo linalohusu Ujerumani kwa ujumla.

Kauder amesema ni aibu kwamba taasisi za Kiyahudi nchini Ujerumani lazima zilindwe na polisi na kwamba Wayahudi mara nyingi wanaogopa kutoka nje na kusema hadharani kwamba wao ni Wayahudi. "Hilo ni jambo lisilovumilika," aliongezea Kauder.

Rais wa baraza kuu la Wayahudi Ujerumani, Josef Schuster ameukaribisha mpango wa kuwepo na kamishna wa kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi. Ameliambia shirika la habari la Ujerumani, epd kuwa ana hofu kubwa juu ya chuki dhidi ya Wayahudi inayoonekana katikati ya jamii.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema kamishna atakayeongoza tume ya chuki dhidi ya Wayahudi hatofanikiwa. Miongoni mwa wakosoaji hao ni mwanahistoria wa Ujerumani mwenye asili ya Israel, Michael Wolffsohn na Petra Pau, naibu spika wa bunge la Ujerumani na mbunge wa chama cha Die Linke. Wamesema pendekezo hilo linaweza lisizingatie haki, kwa kuwa inaliweka tatizo la wimbi la wahamiaji katika kiini cha mzozo huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DW http://bit.ly/2rme4uI
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman