1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yaokolewa kwa mara ya tatu

Admin.WagnerD21 Agosti 2015

Bunge la Ujerumani limeupitisha kwa kura nyingi mpango wa tatu wa kuiokoa Ugiriki. Wabunge 454 walipiga kura ya ndio, 113 waliupinga na 18 hawakupiga kura. Hata hivyo Ugiriki inatakiwa iyaharakishe mageuzi

https://p.dw.com/p/1GHrm
Bunge la Ujerumani mjini Berlin
Bunge la Ujerumani mjini BerlinPicha: Reuters/F. Bensch

Akiwahutubia wabunge kabla ya kura kupigwa Waziri Schäuble aliwahimiza wabunge wauunge mkono mpango huo wa tatu wa kuiokoa Ugiriki. Schäuble alisema kuupitisha msaada huo wa jumla ya Euro Bilioni 86 ni kwa ajili ya maslahi ya pamoja ya Ugiriki na Ulaya . Lakini wakati huo huo Waziri Schäuble ameitaka Ugiriki iyatekeleze iliyoahidi kwa nchi nyingine za ukanda wa sarafu ya Euro.

Schäuble alitahadharisha kwa kusema isingekuwa hatua ya kuwajibika kuipoteza fursa ya kuleta mwanzo mpya baada ya Bunge la Ugiriki kuiunga mkono sehemu kubwa ya hatua za mageuzi ambayo, wakopeshaji wa kimataifa wanataka Ugiriki iyafanye.

Spika wa Bunge la Ujerumani Nobert Lammert alifahamisha kwamba wabunge 454 waliuridhia mpango huo,113 waliupinga na 18 hawakupiga kura.Bunge la Ujerumani lina jumla ya wabunge 585.

Ugiriki yatakiwa kuchukua hatua zaidi

Akizungumza baada ya wabunge kuupitisha mpango huo Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble ameitaka Ugiriki ichukue hatuaza haraka kwa ajili ya kuleta mageuzi. Amesema kadri serikali ya Ugiriki itakavyochelewa kuzichukua hatua hizo ndivyo mambo yatakavyokuwa magumu baadae.Lakini amesisitiza kwamba mageuzi hayo ni ya lazima hasa nchi ikiwa ni mwanachama wa umoja wa kisarafu.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble
Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang SchäublePicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Hata hivyo chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto kimeupinga mpango huo wa tatu wa kuiokoa Ugiriki.Kiongozi wa wabunge wa chama hicho Gregor Gysi amesema mpango huo unaweza kusababisha umasikini zaidi kwa wagiriki.

Lakini kutokana na kuungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge wa chama cha Kansela Merkel kinachoiongoza serikali ya mseto ,CDU ,na kutokana na kuungwa mkono na wabunge wa chama cha Social Demokratik,SPD kilichomo katika serikali hiyo mpango wa tatu wa kuiokoa Ugiriki ulipitishwa kwa urahisi.

Bado viunzi vipo njiani

Mpango wa kuiokoa Ugiriki pia unatarajiwa kupitishwa na mabunge ya nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya.Wabunge wa Uhispania, Estonia na Austria waliuridhia hapo jana. Wabunge wa Uholanzi wanapiga kura leo.

Mkataba juu ya mpango wa tatu wa kuisaidia Ugiriki unapaswa uviruke viunzi vyote ili nchi hiyo iweze kupatiwa fungu la kwanza la fedha na hivyo iweze kulilipa deni lake la Benki Kuu ya Ulaya ECB hapo kesho.

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/P. Tzamaros

Kulingana na masharti ya mkataba huo,Ugiriki inatakiwa ichukue hatua zaidi za kubana matumizi,ipandishe kodi na ifanye mageuzi makubwa katika sekta yake ya uchumi. Uchumi wa Ugiriki ulikuwa umeshuka katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amesema ikiwa Ugiriki itayatekeleza masharti yote kwa moyo wote uchumi wake utastawi tena.Schäuble amesema fursa hiyo ipo, na kuongeza kuwa sasa ni juu ya Wagiriki kuitumia fursa hiyo. Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tspras anatafakari kuitisha kura ya imani baada ya wabunge wengi wa chama chake kuupinga mpango wa kuuokoa uchumi wa nchi hiyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/ape,dpa,

Mhariri: Daniel Gakuba