1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani na mzozo wa Marekani na Iran Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Oktoba 2017

Kikao cha kwanza cha bunge la Shirikisho, Bundestag, mvutano kati ya Marekani na Iran na ripoti kuhusu hali ya umaskini miongoni mwa watoto nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini

https://p.dw.com/p/2mOYC
Bundestagssitzung Bundestag Berlin
Picha: Reuters/

Tunaanzia Berlin, mji mkuu wa Ujerumani ambako bunge jipya linafunguliwa. Ni la kwanza la aina yake tangu kupita karibu miaka 60. Vyama sita vya kisiasa vinawakilishwa na miongoni mwao kinakutikana kile cha siasa kali za mrengo wa kulia, "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani"-AfD. Wahariri wanakubaliana ule utaratibu uliokuwa ukifuatwa hadi wakati huu bungeni, utabadilika. Mhariri wa gazeti la "Badische Neuste Nachrichten" anaandika: "Kipindi cha utulivu kimeshamalizika. Na kwa namna hiyo zimemalizika pia enzi za utawala usiokuwa na pupa wa serikali ya muungano wa vyama vikuu, serikali ambayo kutokana na wingi wao mkubwa wa viti katika bunge la shirikisho Bundestag-asili mia 80, ilikuwa na uwezo wa kufanya vyovyote vile walivyokuwa wakitaka.. Katika bunge linalofunguliwa leo hii, hali itakuwa nyengine kabisa, mijadala moto moto na malumbano ndio yanayotarajiwa kugubika vikao vya bunge hilo. Na kama kweli serikali ya muungano wa Jamaica itaundwa, basi serikali hiyo itakabiliana na upinzani mkali, tangu wa kutoka mrengo wa kushoto mpaka mrengo wa kulia."

AfD wanataka wadhifa bungeni,jee wapewe?

Kishindo kitaanza tangu leo wakati wa kumchagua spika wa bunge la shirikisho na wasaiidizi wake.Gazeti la "Saabrücker Zeitung" linaandika: "AfD watashinda ikiwa mgombea wao, Albrecht Glaser, atashindwa hii leo.Watajinata kwa kusema "mnaona jinsi mfumo wa vyama visivyoheshimu haki, unavyotutendeya. Wanatupokonya haki yetu...na kadhalika. Lakini walio wengi wana njia nyengine pia ya kutompigia kura Glaser bila ya kuwapatia AfD fursa ya kudai wanaonewa: wanaweza kujizuwia kupiga kura."

Siasa ya nje ya Marekani yawageukia wnyewe

 Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani "Hannoversche Allgemeine" linamulika siasa ya nje ya Marekani  kwa kuzingatia mvutano pamoja na Iran. Gazeti linaandika: "Siasa ya nje ya rais wa Marekani Donald Trump imewageukia wenyewe. Kwa kujaribu kutangaza marufuku ya kuingia nchini humo na hasa kwa waumini wa dini ya kiislam, wengi wamepoteza imani yao kwa Marekani. Na dalili nyengine ni ule uamuzi wa Marekani wa kuzidisha sana bajeti ya ulinzi na badala yake kupunguza kwa thuluthi moja ile ya wizara ya mambo ya nchi za nje imezusha hofu kuelekea Marekani. Ili kuzuwia kitisho cha hali kuzidi kuwa mbaya Mashariki ya kati kwa mfano, matarajio ya walimwengu yanaelekezwa Ulaya. Katika wakati kama huu ambapo hali ya usalama iko mashakani, walimwengu wanahitaji dalali  mkweli na wa kuaminika ."

Umaskini wawaathiri watoto Ujerumani

 Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika ripoti iliyochapishwa humu nchini na kuzungumzia juu ya hali ya umaskini miongoni mwa watoto. Gazeti la "Aachner Nachrichten" linaandika: "Maskini anaendelea kuwa maskini. Hilo si jipya. Mashirika ya ustawi wa jamii, shirika la hifadhi ya watoto na vyama vya wafanyakazi kwa miaka sasa wamekuwa wakiwasihi wanasiasa wapambane na umaskini na hasa miongoni mwa watoto. Wametoa mapendekezo na mikakati kuandaa jinsi ya kupambana na hali hiyo. Lakini hadi wakati huu hakuna serikali yoyote iliyofanikiwa. Serikali kuu na zile za majimbo zimesalia kutupiana lawama. Kinachoathirika ni juhudi za pamoja za jamii za kubuni mkakati madhubuti wa kuupiga vita umaskini miongoni mwa watoto. Wanaoathirika  zaidi hapo ni mamilioni ya watoto na vijana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman