1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya laidhinisha Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya

Daniel Gakuba
27 Novemba 2019

Bunge la Ulaya limeidhinisha wajumbe wapya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, inayoshughulikia masuala ya kila siku ya uongozi wa umoja huo. Kwa kura hiyo, Ursula von der Leyen ataanza majukumu yake Jumapili ijayo.

https://p.dw.com/p/3Tq2D
Sitzung Europäisches Parlament - Wahl EU-Kommission Ursula von der Leyen
Ursula von der Leyen, Rais mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa UlayaPicha: Reuters/V. Kessler

Kabla ya bunge la Ulaya mjini Strasbourg kuwapigia kura makamishna 27 aliowapendekeza, Ursula von der Leyen alikuwa ametoa ahadi ya kufanya mageuzi ambayo amesema yatafika katika kila kona ya jamii na ya uchumi wa Ulaya. Kura ilipopigwa, wabunge 461 waliunga mkono makamishna waliopendekezwa, huku 157 wakipiga kuwakataa, na 89 walijizuia.

Karibu nusu ya makimishna hao 27, Von der Leyen akiwemo, ni wanawake, na hilo amesema inadhihirisha hatua iliyopigwa katika kuendeleza usawa wa jinsia, ingawa bado yapo mengi ya kufanya.

Umoja kwa maslahi ya Ulaya

Belgien | Von der Leyen stellt zukünftige Kommission vor
Bi Ursula von der Leyen katika picha ya pamoja na baadhi ya wasaidizi wakePicha: picture-alliance/dpa/AP/V. Mayo

Bi Ursula von der Leyen ambaye kabla ya kuchaguliwa katika wadhifa huu mpya alikuwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani, amesema halmashauri anayoiongoza itafanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya Umoja wa Ulaya.

''Kwa pamoja, tutafanya kazi kwa maslahi ya pamoja ya Ulaya. Tutafanya kazi kama timu moja na bunge hili, pamoja na nchi wanachama, kukabiliana na changamoto zinazokikabili kizazi cha leo. Tuko tayari, lakini la muhimu zaidi, Ulaya iko tayari. Ujumbe wangu ni huu: twende kazini.'' Amesema von der Leyen

Miongoni mwa makamishna wapya 27, wamo manaibu-kamishna watatu, ambao ni Valdis Dombrokvskis kutoka Latvia, Frans Timmermanns kutoka Uholanzi, na Margrethe Vestager kutoka Denmark.

Mazingira miongoni mwa vipaumbele

Frankreich Jean-Claude Juncker im EU-Parlament
Jean Claude Juncker, Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya anayemaliza muda wakePicha: AFP/F. Florin

Von der Leyen amesema masuala ya kipaumbele wakati wa uongozi wake yatakuwa utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kuimarisha miundombinu na mfumo wa digitali, na Ulaya kutoa mchango muhimu zaidi kwenye jukwaa la ulimwengu. Kuhusu utunzaji wa mazingira, rais huyo mpya wa Halmashauri Kuu ya Ulaya amesema hakuna tena muda wa kupoteza.

Amesema, ''Kadri tutakavyoharakisha kuchukua hatua, ndivyo wananchi wetu watakavyonufaika, na ndivyo tutakavyoongeza mafanikio na uwezo wetu. Mpango wa kijani wa Ulaya ni lazima kwa afya ya sayari yetu, kwa watu wetu, na kwa uchumi wetu.''

Suala jingine ambalo amesema litafuatiliwa kwa karibu na la wahamiaji. Von der Leyen amesema wahamiaji watakaokubaliwa kubaki Ulaya watajumuishwa katika jamii, lakini wale watakaokataliwa, watarudishwa walikotoka.

Awali bunge la Ulaya liliwakataa watu watatu waliokuwa wamependekezwa na Ursula von der Leyen kuwa makamishna, wakitoka Ufaransa, Romania na Hungary, na nchi zao zililazimika kutafuta watu wengine. Mchakato huo ulimchelewesha Von der Leyen kuanza majukumu yake kwa mwezi mzima.

dpae, rtre