1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uturuki kuanza leo shughuli za kumchagua rais

20 Agosti 2007

Kufuatia ushindi mkubwa wa chama cha AKP katika uchaguzi wa Julai 22 nchini Uturuki chama hicho kimemteua kwa mara nyingine tena waziri wa mambo ya nje Abudullah Gul kugombea kiti cha rais.

https://p.dw.com/p/CB1v
Bendera ya Uturuki
Bendera ya Uturuki

Bunge la Uturuki linatarajiwa kumchagua rais katika takriban awamu nne za kura, ya kwanza ikifanyika hii leo.

Chama kinachotawala cha Uturuki cha AKP kilimchagua bwana Gul kwa mara ya kwanza kuwania kiti hicho cha urais mwezi wa April na hatua hiyo ilizusha mzozo wa kisiasa nchini humo uliosababisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kufanya maandamano ya kuunga mkono siasa zisizo fungamana na dini.

Chama cha AKP kililazimika kuitisha uchaguzi wa mapema na katika uchaguzi huo wa Julai 22 chama hicho cha AKP kikashinda kwa kura nyingi.

Makamu mwenyekiti wa chama cha AKP bwana Saban Disli amesema ushindi huo ulitoa nafasi mpya ya kuteuliwa tena bwana Gul kugombea kiti cha urais na chochote kinyume na hivyo itakuwa sawa na kukiuka mapenzi ya wapiga kura.

Bwana Gul ana umri wa miaka 56 na tangu alipokuwa chuo kikuu alijiunga na vyama vya kisiasa vya kiislamu.

Mwaka 1983 hadi mwaka 1991 alikuwa mwanauchumi katika benki ya maendeleo ya kiislamu mjini Jeddah Saudi Arabia.

Mwaka 1991 alijiunga rasmi na siasa na alikuwa naibu mwenyekiti wa chama cha kiislamu cha Islamic Welfare Party.

Alichukuwa wadhfa wa waziri wa nchi na msemaji wa serikali ya Erbakan mnamo mwaka 1996 lakini serikali hii iling’olewa madarakani kufuatia kampeni za kisiasa zilizoungwa mkono na jeshi mwaka 1997.

Lakini licha ya hayo bwana Abdullah Gul anaheshimika duniani kote kuwa ni mtu mwenye msimamo kadirifu na mwenye kuunga mkono mageuzi na mwanasiasa aliye karibu sana na umoja wa ulaya hasa katika kipindi cha miaka minne alipohudumu kama waziri wa mambo ya nje katika serikali ya chama cha AKP.

Wakati akiwa waziri wa mambo ya nje, Uturuki ilianzisha uhusiano wenye mtazamo mpya kati yake na nchi za kiarabu na za kiislamu.

Licha ya utendaji kazi wa bwana Gul kuonekana wazi na mawazo yake kadirifu yakijulikana na wengi katika nchi za magharibi lakini nchini mwake Uturuki walio na msimamo wa kutenganisha siasa na dini wanaamini kuwa hiki ni kitendawili tu na chama cha AKP kina malengo ya kuvunja msimamo huo wa taifa la Uturuki.

Naibu wmenyekiti wa chama cha Republican Peoples Partry Onur Oymen anapinga kuchaguliwa bwana Gul kuwa rais wa Uturuki.

Jeshi la Uturuki hata hivyo linasema kutokana na ushindi mkubwa wa chama cha AKP cha muhimu kwa sasa ni kusubiri na kuangalia mambo yatakavyo kuwa.