1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Marekani laimulika NSA kwa kulidukuwa

Admin.WagnerD31 Desemba 2015

Kamati ya uchunguzi ya baraza la wawakilishi la Marekani imelitaka shirika la usalama wa taifa NSA, kutoa taarifa kuhusu ripoti kwamba shirika hilo lilinasa mawasiliano kati ya maafisa wa Waisrael na wabunge wa Marekani.

https://p.dw.com/p/1HWa9
NSA Symbolbild
Picha: picture-alliance/dpa

Katika barua iliyotumwa kwa mkurugenzi wa NSA Michael Rogers, mwenyekiti wa kamati ya usimamizi Jason Chaffetz na mwenyekiti w akamati ndogo Ron DeSantis, walisema habari iliyotokea katika toleo la Jumanne la jarida la Wall Street iliibua maswali kuhusu utaratibu unaofuatwa na wafanyakazi wa NSA katika kuanisha iwapo mawasiliano yaliyonaswa yanawahusisha wabunge wa bunge la Marekani Congress.

Jarida hilo, likiwanukuu maafisa wa sasa na wa zamani wa serikali ya Marekani, lilisema NSA ilikuwa ikimlenga waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wa Israel baada ya kuanzisha kampeni yao katika bunge la Marekani kujaribu kukwamisha makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Sambamba na kunasa mawasiliano ya maafisa wa serikali ya Israel, uchunguzi huo ulinasa pia taairfa za ndani kuhusu juhudi zao za uraghibishi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mazungumzo yao na wabunge wa Congress na makundi ya Wayahudi wa Marekani, liliripoti jarida hilo.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Getty Images/C. Koall

Barua kutoka kwa Chaffetz na DeSantis, wote kutoka chama cha Republicans, ilimtaka Rogers kuwapatia taarifa juu ya utaratibu wa shirika hilo kuamua iwapo mawasiliano ya wabunge yamenaswa katika udukuzi wa NSA, na kwa kiasi gani wafanyakazi w ashirika hilo wamekuwa wakitoa taarifa hizo kwa mashirika mengine ya Marekani pamoja na ikulu ya White House.

Kamati hiyo pia iliitaka NSA iipe maelezo mafupi kuhusu wafanyakazi wake. Jarida la Wall Street liliripoti kuwa NSA ilifuata muongozo unaozitaka ripoti zake za uchunguzi kuondoa majina yoyote ya Wamarekani, wakiwemo wabunge, waliotajwa katika mawasiliano ya Waisrael yalionaswa.

Ripoti ya Jarida hilo ilisema hata baada ya rais Barack Obama kutangaza miaka miwili iliyopita kuwa angeweka ukomo kwenye kuyachunguza mataifa washirika, NSA iliendelea kumchunguza waziri mkuu wa Israel Banjamini Netanyahu pamoja na maafisa wa ngazi za juu nchini humo.

Ikulu ya White House ilikataa kuzungumzia shughuli zozote makhsusi za kijasusi zilizofanywa na Marekani. Lakini maafisa wa White House walisema Marekani haifanyi uchunguzi nje ya nchi mpaka pawepo na sababu ya usalama wa taifa inayoisukuma kufanya hivyo, na kusisitiza kuwa kanuni hiyo inatumika kwa viongozi wa dunia na raia wa kawaida.

Na katika juhudi za kuonyesha kuwa uhusiano wa kiulinzi kati ya Marekani na Israel haujaathiriwa na ripoti hizo, maafisa walibainisha kuwa maafisa wa Marekani walisafiri kwenda Israel mwezi huu kuanzisha tena mazungumzo ya makubaliano mapya ya miaka 10 kuhusu msaada wa kijeshi wa Marekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman