1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi kujiondowa ICC

Sylvia Mwehozi
7 Oktoba 2016

Baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuonesha dhamira ya kuchunguza matukio ya uvunjwaji wa haki za binaadamu na mauaji nchini Burundi, sasa serikali ya nchi hiyo inasema inataka kujitoa ICC.

https://p.dw.com/p/2R0YD
Burundi Pierre Nkurunziza
Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Makamu wa Rais wa Burundi, Gaston Sindimwo, anasema nchi yake ina mpango wa kujiondoa kutoka ICC, ikiwa ni miezi sita baada ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou Bensouda, kusema watachunguza ghasia zilizozuka nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Sindimwo amesema tayari serikali ya Burundi imeiandikia ICC kueleza nia yao ya kujiondoa kutoka Mkataba wa Roma ulioiunda, kwani wamegundua "ni muhimu kujiondoa ili Burundi iwe huru."

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilitumbukia katika mzozo mwaka jana baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kugombea muhula wa tatu madarakani kinyume na katiba, kwa mujibu wa wapinzani wake.