1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi: Upinzani Burundi wadai wanachama wao 55 wamekamatwa

Amida Issa23 Septemba 2020

Wafuasi 55 wa chama kikuu cha upinzani Burundi CNL wamekamatwa katika kipindi kisichozidi wiki 2.

https://p.dw.com/p/3isdT
Burundi Coronavirus - Präsidentschaftswahl | Agathon Rwasa
Picha: picture-alliance/AP/D. Nininahazwe

Mkuu wa chama hicho Agathon Rwasa amesema kamatakamata hiyo inaendeshwa dhidi ya wafuasi wake wakishukiwa kuhusika katika uasi unaofukutia, wakati wao hawahusiki.

Baraza la kitaifa la usalama lilibaini kuwepo na watu wenye silaha wanaoingia katika mkoa wa Rumonge kusini mwa Burundi kupitia Ziwa Tanganyika wakitokea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.


Mkuu wa chama cha CNL, Agathon Rwasa amesema wafuasi wake wamekuwa wakikamatwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, kwa tuhuma za kuongoza mikutano kinyume cha sheria. Rwasa amesema katika mkoa wa Bururi wafuasi wa chama hicho walikamatwa wakiwa katika ofisi ya chama katika mkutano wao wa kawaida.

Agathon Rwasa akanusha madai ya chama chake kuhusika na uasi

Mwanasiasa Agathon Rwasa amesema chama chake hakihusiki na uasi huo na kwamba hakuna sababu ya kuwaandama wafuasi wa chama chake wakati wahusika wa uasi huo tayari wamejitangaza.

Burundi Wahlen
Picha: Getty Images/AFP

Mkoani Rumonge wafuasi wa CNL waliotiwa nguvuni walituhumiwa kukipigia debe chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi ulofanyika Mei mwaka huu na kwamba kumekuwepo na  baadhi ya watawala wanawashurutisha wafuasi wa chama chake kuhamia chama tawala.

 


Amnesty Int: Burundi ishughulikie haki za binadamu

Hali hiyo inajitokeza wakati kumekuwa na taarifa za kuwepo na uasi unaofukuta nchini. Mkoani Rumonge watu zaidi ya 20 tayari wameuwawa mnamo ziku za nyuma katika matukio tofauti ya mashambulizi ya watu wenye silaha.

Baraza la kitaifa la usalama liliwataka watawala katika mkoa huo wa Rumonge, unaopakana kwa sehemu kubwa na Ziwa Tanganyika kuwakagua wavuvi wanaoingia kwenye ziwa hilo kwa shuhuli za uvuvi.

Na kwamba wanaoushambulia mkoa huo huingia nchini kupitia Ziwa Tanganyika wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. CNL ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Burndi na kilichoyapinga matokeo ya uchaguzi wa Mei na kushika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita hakijashirikishwa katika taasisi za serikali.