1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yaingia kwenye mgogoro wa kisiasa

6 Februari 2014

Burundi imetumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya mawaziri watatu wa chama cha Uprona ambacho wafuasi wake wengi ni kutoka kabila ya Watutsi kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/1B3Xd
Präsidentenwahlen in Burundi - Pierre Nkurunziza
Picha: picture alliance/dpa

Hatua ya mawaziri hao inavuruga utaratibu wa kugawana madaraka baina ya Wahutu walio wengi nchini humo na jamii ya wachache ya Watutsi, jamii ambazo zimekua kwa miongo mingi zikijaribu kufikia maridhiano.

Chama cha Uprona kimesema Waziri wa Maendeleo ya Tarafa, Jean Claude Ndihokubwayo, Waziri wa Mawasiliano, Leocide Nihaza, na Waziri wa Biashara, Victoire Ndikumana, walijiondoa serikalini.

Msemaji wa chama hicho, Tatien Sibomana, amesema wanakataa kushirikiana na chama cha CNDD-FDD cha Rais Pierre Nkurunziza, kwani "kina mkakati wa kuiangamiza Uprona."

'Hujuma' za CNDD-FDD

Kujiuzulu kwa mawaziri hao kunafuatia shutuma za Uprona kwamba chama cha CNDD-FDD kilikula njama za kumuondoa mwenyekiti wa Uprona, Charles Nditije, kwenye nafasi yake kabla ya uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika mwaka 2015 na badala yake kumuweka mtu anayeonekana kuwa ni mfuasi wa Nkurunziza.

Kiongozi wa zamani wa waasi wa Burundi, Agathon Rwasa.
Kiongozi wa zamani wa waasi wa Burundi, Agathon Rwasa.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, msemaji wa Rais, Willy Nyamitwe, alipuuzia madai kuhusika kwa Rais Nkurunziza na chama chake katika mgogoro uliokikumba chama cha Uprona, akisisitiza kwamba kumekuweko na migogoro na hali ya kutofahamiana.

Alisema Nkurunziza bado hajatangaza kwamba atakuwa mgombea katika uchaguzi ujao. "Acha tusubiri 2015," alisema Nyamitwe.

Kiongozi wa mashirika ya kiraia, Pacifique Nininahazwe, amesema Rais Nkurunziza atafanya kila awezalo abakie madarakani muhula wa tatu.

Athari za kujiondoa Uprona serikalini

Uprona ndicho chama pekee, baada ya CNDD-FDD, ambacho hakikususia uchaguzi wa 2010 nchini Burundi. Vyama vyengine vyote vililalamika kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa udanganyifu na wizi wa kura.

Rais Pierre Nkuruzinza akitembelea Iran.
Rais Pierre Nkuruzinza akitembelea Iran.Picha: FARS

Mbali na mawaziri hao watatu, Uprona kilikuwa pia na Makamu wa Rais, Bernard Busokoza, katika serikali hiyo, ambaye pia aliondolewa kufuatia kuukosoa mpango wa Nkurunziza kuibadili katiba ili aweze kugombea muhula wa tatu na jinsi anavyoishughulikia migogoro ya ardhi nchini humo.

Mvutano kuhusu suala la ardhi umepamba moto, huku Wahutu wanaorejea nyumbani mara nyingi wakiwa wamedai ardhi ambazo zinamilikiwa na wenzao Watutsi. Tume ya serikali iliopewa jukumu la kutafuta suluhu, imekuwa ikilaumiwa katika miezi ya karibuni kwa kuwapendelea Wahutu.

Afisa mmoja wa ubalozi wa kigeni ambaye hakutaka kutajwa jina, alionya kwamba mgogoro huu unaweza ukapamba moto zaidi, na ni jambo linalotia wasiwasi kwa sababu kuishambulia Uprona ni kuishambulia jamii ya Watutsi.

Historia ya Burundi imekumbwa na uhasama wa kikabila na mauaji yaliyotokea 1972 na 1988, pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Rais wa kwanza Mhutu kuchaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye, aliuwawa na wanajeshi wa Kitutsi mwaka 1993 na tukio hilo kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef