1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yapuuza ukosoaji wa vikosi vyake

Admin.WagnerD16 Desemba 2015

Burundi imepuuzilia mbali ukosoaji dhidi ya vikosi vyake vya usalama, na kusema vinafanykazi kwa weledi, ikimesema pia hakuna haja ya kutuma walinda amani wa kigeni nchini humo.

https://p.dw.com/p/1HO83
Burundi Soldaten Sicherheitskräfte Militär
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kuroawa

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UNSC limezungumzia hatua zinazojumlisha kutuma kikosi cha kulinda amani kushughulikia mgogoro wa Bunrundi, ambao unawapambanisha wafuasi wa rais Pierre Nkurunziza dhidi ya wapinzani wa muhula wake wa tatu madarakani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliliambia baraza la usalama mwezi uliyopita kuwa Burundi ilikuwa kwenye kingo za vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini akasema hakuna haja ya kupeleka haraka walinda amani wa Umoja wa Mataifa, na kuliomba baraza hilo kuzingatia njia nyingine.

Katika tukio la karibuni la kuchacha kwa mgogoro huo, watu wenye silaha walivamia kambi za kijeshi siku ya Ijumaa iliyopita. Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al Hussain alisema siku ya Jumanne kuwa serikali imejibu mashambulizi kwa kuanzisha msako wa nyumba hadi nyumba, kuwakamata watu kiholela na madai ya mauaji ya chapchap. Mapigano hayo yaliuawa karibu watu 90.

Msemaji wa serikali ya Burundi Willy Nyamitwe.
Msemaji wa serikali ya Burundi Willy Nyamitwe.Picha: DW/J-C Abalo

'Hatuhitaji walinda amani'

Taarifa ya serikali iliyotolewa jana, ilisema vikosi vya usalama viliingilia kati kwa weledi wa hali ya juu sana, na kwamba haileti maana kuzungumzia kuleta wanajeshi wa kigeni nchini Burundi. Taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wa serikali ya Burundi iliongeza kuwa wale wanaopendekeza jambo hilo wana mengi wanayoyaficha.

Burundi imeituhumu nchi jirani ya Rwanda na baadhi ya mataifa ya magharibi kwa kuingilia masuala yake ya ndani, ikisema wanachochea mgogoro katika taifa hilo maskini la Afrika. Katika taarifa nyingine, chama tawala cha Burundi CNDD-FDD, kilimtuhumu mkoloni wa zamani wa taifa hilo Ubelgji, kwa kutoa silaha kwa magaidi na kuwasaidia kitabibu wanapojeruhiwa.

Maafisa kadhaa wameitoroka na Burundi na kukimbilia Ubelgji tangu kuripuka kwa mgogoro wa sasa. Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yameelezea wasiwasi unaozidi kwamba Burundi, ambayo ilitoka kwenye vita mwaka 2005, huenda ikatumbukia tena kwenye mgogoro wa kikabila, na kuivuruga kanda ambayo tayari ilishuhudia mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. Kama ilivyo kwa Rwanda, Burundi pia Kabila na Wahutu walio wengi na Watutsi wachache.

Watu wakibeba maiti ya mtu alieuawa katika mashambulizi ya hivi Karibuni mjini Bujumbura.
Watu wakibeba maiti ya mtu alieuawa katika mashambulizi ya hivi Karibuni mjini Bujumbura.Picha: picture-alliance/AP Photo

AU yaelezea wasiwasi pia

Wachunguzi wa haki za binaadamu wa Umoja wa Afrika wameelezea pia wasiwasi mkubwa kuhusiana na kuongezeka kwa vurugu nchini humo, baada ya kushuhudia baadhi ya mapiganao makali zaidi nchi humo katika kipindi cha miezi kadhaa.

Timu ya Kamisheni ya Haki za binaadamu inayoungwa mkono na Umoja wa Afrika ilikuwa nchini Burundi kuanzia Desemba 7 hadi 13 kwa uchunguzi. Tume hiyo imeelezea kupotea taarifa za ukiukaji wa haki za binaadamu unaoendelea pamoja na ukiukaji mwngine ukiwemo mauaji ya kiholela na mauaji ya kulenga, kukamatwa watu hovyo na kuwekwa vizuwizini, mateso, kusimamishwa kazi kiholela na kufungiwa kwa baadhi mashirika ya kiraia na vyombo vya habari.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman