1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Bush anajiweka juu ya sheria"

Maja Dreyer4 Julai 2007

Kwanza katika udondozi wa leo tunaelekea Marekani na kusikiliza tathmini juu ya hatua ya rais Bush ya kumpa msamaha afisa wa juu wa zamani wa ikulu ya Marekani “White House”, Lewis Libby.

https://p.dw.com/p/CHSW

Gazeti la “Rheinische Post” limeandika yafuatayo:

“Rais Bush anaingilia katika mambo ya mahakama. Kashfa ni kwamba Bush anajiweka juu ya sheria. Uhuru wa sheria hauzingatiwi ikiwa rais anachukua hatua ya kisiasa. Kisa cha afisa Libby kimegonga vichwa vya habari, kwa sababu kimeweka wazi udanganyifu wa serikali ya Marekani katika kutoa sababu kuanzisha vita dhidi ya Saddam Hussein wa Iraq mnamo mwaka 2003. Picha inayoonekana sana ni kwamba, rais anajaribu kuficha udanganyifu kwa sababu ni rafiki yake wa kisiasa.”

Na mhariri wa gezeti la “Süddeutsche Zeitung” pia ana wasiwasi juu ya uamuzi wa rais Bush:

“Rais kumpa msamaha, hasa kwa rafiki wake, si kitu kipya katika mfumo wa mamlaka wa Marekani. Kinachokasirisha lakini ni mambo mawili: Kwanza rais anaingilia katikati ya utaratibu wa kisheria ambao haujamalizika, yaani bado kuna uwezekano wa kisheria wa kupinga hukumu iliyotolewa. Hivyo, rais anauathiri uaminifu wa mfumo wa sheria. La pili ni kwamba, Bush hampi msahama kabisa Lewis Libby, kwani hukumu bado ipo. Ni adhabu ambayo Bush amebadilisha. Kwa hivyo rais huyu amechukua nafasi ya baraza la wazee wa mahakama, anachukua nafasi ya umma!”

Rais Bush wa Marekani jana pia alimuuaga mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, ambaye alimtembelea kwenye nyumba yake ya likizo. Matokeo ya mkutano huu yanachambuliwa na gazeti la “Financial Times Deutschland”:

“Tukitoa muhtasari wa ziara hiyo ya Putin kwake Bush tunaweza kusema: Putin ameweza kuvua samaki, Bush ameshindwa. Yaani picha hii inafaa kwa safari yao ya boti ambayo marais hao wawili wamefanya, na pia kuhusiana na mazungumzo yao ya kisiasa. Pale Bush alijirudia katika mvutano juu ya mitambo ya kukinga makombora barani Ulaya, Putin alikuwa na pendekezo jipya la kwamba Wamarekani wanaweza kutumia mtambo mmoja wa Kirusi ikiwa itakubali kuachana na mpango wake wa kujenga mitambo mipya katika nchi za Poland na Jamhuri ya Chek.”

Na mwisho tunarudia humu nchini ambako jana, mahakama ya shirikisho ya taifa imeamua kuwa kutumwa kwa ndege za Kijerumani za kivita, aina ya Tornado huko Afghanistan inaenda sambamba na sheria. Chama cha mrengo wa kushoto kilitoa shtaka dhidi ya hatua hiyo. Mhariri wa “Neue Osnabrücker Zeitung” anaisifu mahakama kwa uamuzi huo:

“Ni hukumu ya busara. Kwani uhuru wa bunge kuamua juu ya masuala ya matumizi ya jeshi hautegemei jeshi litatumia vyombo gani katika hatua yake. Inabidi tu silaha au vyombo vifae hali ilivyo. Ndege za aina ya Tornado zinahitajika Afghanistan,kwa hivyo ni sawa zitumike huko. Ikiwa mahakama ingeamua tofauti, uwezo wa Ujerumani kuchukua hatua kwenye jukwaa la kimataifa ungepunguzwa sana.”

Na hatimaye juu ya suala hilo ni gazeti la “Handelsblatt”ambalo linataja wasiwasi mwingine:

“Hatua ya kijeshi nchini Afghanistan inaonekana kama haifanikiwi. Mahakama ya katiba ya Ujerumani ni mahala panapopaswa matatizo yatatuliwe. Wala sio bunge la Ujerumani, kwani kinachozungumziwa hapa ni mchango wa Ujerumani tu. Ni juu ya jumuiya ya NATO na pia serikali ya Washington ambazo zinasimamia operesheni hizo mbili. Hadi sasa mikakati yao haiendi sambama.”