1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush apwaya mbele ya baraza kuu la Umoja wa mataifa mjini New-York

Nehls, Thomas / New York (WDR) 24 Septemba 2008

Mashirika ya fedha yanabidi kufuata maadili na kuwajibika anasema mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya Nicolas Sarkozy

https://p.dw.com/p/FO3v
Rais George W. Bush akinyanyua bilauri yake katika karamu ya chakula cha usiku katika makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New-YorkPicha: AP


Mjadala wa 63 wa baraza kuu la umoja wa mataifa umeanza jana mjini New-York.Safari hii mjadala huo umegubikwa na mzozo wa fedha.Dunia haikabiliwi pekee na mizozo ya fedha,nishati na vyakula,anasema katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon, inakosa pia uongozi jumla wenye nguvu.Ushahidi mzuri wa hali hiyo ni ile hotuba iliyotolewa na mtu ambae,kimsingi amejitokeza kutwaa dhamana hiyo ya uongozi.


Tofauti kati yao ni kubwa kupita kiasi.Huku unamkuta mwanasiasa mwenye nguvu kupita kiasi aliyesaliwa na miezi minne madarakani na ambae hakuona umuhimu wa kutumia hata sekondi moja kuwapa nasaha walimwengu.Na hapo hapo akahutubia  wa pili aliyeonekana kua mtu aliyeitambua hali ya mambo namna ilivyo.Wa mwanzo ni George W. Bush na wa pili ni Nicolas Sarkozy.


Kwamba rais wa Marekani anahutubia kweli kwa muda wa dakika 24 nzima mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa mataifa bila ya hata kutoa ushauri wowote-heko.Hotuba yake mtu anaweza kuitathmini ifuatavyo:mapambano dhidi ya ugaidi lazma yaendelezwe,demokrasia ilindwe na mada nyenginezo za jumla jamala kama hizo.Hotuba yake haikua na uzito wowote.


Aliyekuja kuhutubia baadae lakini,alifafanua kasoro zilizoko.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ameombwa na rais wa Ufaransa,ambae ndie mwenyekiti wa zamu wa umoja wa Ulaya asiyaachie masoko ya hisa kuendesha shughuli zake ovyo ovyo na atilie mkazo pia shughuli za kiuchumi ziambatane na maadili na wajib.


Kama kila alichosema ndo sawa au la-hilo ni suala jengine.Nicolas Sarkozy,rais mwenye machachari wa Ufaransa anataka ubepari ufanyiwe marekebisho haraka na ya kina.Anashauri sio tuu mbinu na mikakati ichunguzwe upya,bali hata wanaadam wajitakase na tamaa na wajiambatanishe na utandawazi.


Kuanzia siku ya mwanzo tuu ya mkutano huo wa 63 wa baraza kuu la Umoja wa mataifa,viongozi wa Nicaragua na mwenzake wa Brazil walipaza sauti .Sauti hizo za sawa zinatoa matumaini na si hasha zikaigizwa na dazeni kadhaa ya viongozi wengine.Waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani,bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul,akishiriki katika mkutano wa ngazi ya juu unaofanyika sambamba na huu wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York,ameonya dhidi ya kutumiwa mikzozo ya fedha kama chanzo cha kuzuwiliwa misaada iliyoahidiwa ya kupambana na umaskini.Nae waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier anapanga kushadidia na hata kulipanua suala hilo.Anapanga kutahadharisha,ikiwa sehemu kubwa ya walimwengu hawatajipatia maji safi ya kunywa,hali hiyo inaweza kuzusha vita.


Mada kama hizo ,ambazo ni za kutafakari,zinawavutia wengi na ziko mstari wa mbele katika ajenda ya mazungumzo ya hadhara kuu ya umoja wa mataifa safari hii.


Mizozo ya fedha  haistahiki kufifiisha uzito wa mizozo ya kisiasa.Na kwakua hadhara kuu ya umoja wa mataifa ni jukwaa la walimwengu-wenye misimamo mikali na wale wenye misimamo ya kibepari,kwa bahati nzuri ni wachache.