1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush asema Iran bado tishio kwa dunia

5 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CXEi

WASHINGTON.Rais George W Bush wa Marekani amesema kuwa Iran bado ni tishio kwa amani duniani.

Amesema hayo mbali na kwamba Idara za ujasusi za nchi hiyo hapo jana zilitoa taarifa ya kwamba Iran ilisitisha mpango wake wa kutengeza bomu la nuklia miaka minne iliyopita.

Rais Bush amesema kuwa taarifa hiyo ni tahadhari juu ya uwezo wa Iran katika kutengeza silaha za nuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Manouchehr Motakki akizungumzia ripoti hiyo amesema kuwa imethibitisha mpango wa nuklia wa nchi hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown pamoja na kutolewa kwa ripoti hiyo amesema kuwa watachagiza kutaka vikwazo zaidi vya kimataifa viongezwe dhidi ya Iran.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Marekani katika kuizuia Iran kuwa na uwezo wa silaha za nuklia.

Lakini mjini Washington wagombea urais wa Marekani kupitia chama cha Democrat, Hillary Clinton, Barack Obama, na John Edward wamesema kuwa ripoti hiyo imefichua uongo wa siasa za Bush juu ya Iran.

China moja ya nchi zenye kura turufu katika Umoja wa Mataifa, imetoa wito kwa mataifa sita makubwa duniani kufikiria upya vikwazo dhidi ya Iran baada ya ripoti hiyo kutolewa.

Mataifa hayo Urusi, China yenyewe, Uingereza, Marekani, Ujerumani na Ufaransa yanakutaka mjini Paris Jumamosi ijayo kuangalia hatua mpya za kuiwekea vikwazo zaidi Iran.