1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameron na Clegg wanaanza kuunda serikali yao ya muungano

Kabogo Grace Patricia12 Mei 2010

Serikali hiyo ijayo ya muungano itakuwa ya kwanza tangu mwaka 1974.

https://p.dw.com/p/NLyw
Waziri Mkuu mteule wa Uingereza, David Cameron, akiwa na mkewe, Bibi Samantha.Picha: AP

Nchini Uingereza Waziri Mkuu Mteule David Cameron na Naibu wake Nick Clegg, wanaanza kuunda sera za serikali yao ya muungano, itakayokuwa ya kwanza tangu mwaka 1974, baada ya vyama vyao Conservative na Liberal Democrats kufikia makubaliano jana na kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa chama cha Labour Gordon Brown. Moja wapo ya changamoto kubwa za serikali ijayo ni kukabiliana na nakisi kubwa katika bajeti ya nchi hiyo.

Chama cha Conservative cha Waziri Mkuu mpya , David Cameron na chama kidogo cha Liberal Democrats leo vinapanga kuunda serikali mpya katika makubaliano baina ya vyama hivyo viwili ambavyo wakosoaji wanasema kuwa vitaipeleka nchi hiyo kwenye matatizo hapo baadae. Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Waziri Mkuu, Cameron alisema kuwa hiyo itakuwa kazi ngumu kwani muungano utaondoa kila aina ya changamoto. Aliongeza kusema kuwa lakini anaamini kwa pamoja vyama hivyo vitafanikiwa kuunda serikali imara ambayo nchi hiyo inahitaji.

''Nadhani huduma ambayo nchi yetu inahitaji kwa sasa ni kukabiliana na changamoto kubwa, kukabiliana na matatizo yetu, kuchukua maamuzi magumu, kuwaongoza watu katika maamuzi hayo magumu, ili kwa pamoja baadae tuweze kufika mahali bora,'' alisema Bwana Cameron.

Makubaliano hayo yalifikiwa siku ya tano baada ya uchaguzi mkuu ambao haukutoa mshindi wa moja kwa moja uliofanyika Alhamisi iliyopita, ambao umemaliza utawala wa miaka 13 wa chama cha Labour baada ya uongozi wa kwanza Tony Blair na baadae mrithi wake Gordon Brown. Serikali ijayo ya muungano itakuwa na jukumu kubwa la msingi la kukabiliana na nakisi kubwa katika bajeti ya nchi hiyo kwa zaidi ya asilimia 11 ya pato la ndani. Serikali hiyo ya muungano inatarajia kutekeleza mipango ya chama cha Conservative ya kupunguza pauni bilioni sita za matumizi ya fedha ya mwaka huu, kuliko ilivyokuwa ikielezwa hapo awali na chama cha Liberal Democrats wakati wa kampeni.

David Cameron bei der Königin Mai 2010
Malkia Elizabeth II wa Uingereza akisalimiana na David Cameron.Picha: AP

Akizungumza na waandishi habari, Nick Clegg ambaye atakuwa Naibu Waziri Mkuu, amesema bila shaka siku zote atafanya kila awezalo kuthibitisha kuwa siasa mpya siyo tu ni rahisi, lakini pia ni bora. Cameron na Clegg, wote wakiwa na umri wa miaka 43, wataiongoza serikali ijayo ya muungano itakayokuwa ya kwanza nchini Uingereza, tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. David Cameron atakuwa Waziri Mkuu mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kuitawala Uingereza tangu karibu miaka 200 iliyopita. Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza kuwa chama cha Liberal Democrats kitakuwa na jumla ya mawaziri watano katika baraza la mawaziri, akiwemo Nick Clegg.

Katika uchaguzi mkuu Alhamisi iliyopita, chama cha Conservative kilishinda kwa kupata viti 306 bungeni, lakini kilikuwa kinahitaji viti vingine 20 ili kupata wingi wa viti 326 katika bunge hilo lenye wabunge 650 kuweza kuunda serikali. Chama cha Labour kilipata viti 258 na Liberal Democrats kilijinyakulia viti 57. Miongoni mwa viongozi wa nchi za nje waliompongeza Bwana Cameron kwa simu baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu jana ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman