1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Castro azikwa, Cuba yaingia kipindi baada ya Fidel

Sekione Kitojo
4 Desemba 2016

Cuba inafunga ukurasa muhimu katika historia yake leo Jumapili (04.12.2016) wakati mazishi ya rais wao wa zamani Fedel Castro yakifanyika na ikitazama siku za usoni bila ya kiongozi huyo aliyetawala kwa miongo  kadhaa.

https://p.dw.com/p/2Ti99
Kuba Trauerfeier Fidel Castro
Mwananchi wa Cuba akikunja picha ya Fidel Castro Picha: Reuters/E. Alonso

Baada  ya  wiki  za  kutoa rambirambi  na  maandamano  ya  umma, majivu  ya  Castro yatazikwa  katika  eneo  la  makaburi  la  Santa Ifigenia  mjini Santiago de Cuba, mji  ulioko  mashariki  mwa  nchi hiyo , ambako  hatua  za  mapinduzi  zilianzishwa  zaidi  ya  nusu karne  iliyopita.

Kuba Trauerfeier Fidel Castro
Majivu ya mwili wa kiongozi wa zamani wa Cuba Fidel Castro yakipitishwa mitaani mjini HavanaPicha: Reuters/E. De La Osa

Rais Raul Castro  aliongoza  mkutano  mkubwa  wa  mwisho  kwa heshima  ya  kaka  yake  katika  eneo  la  uwanja  wa  mapinduzi  wa Santiago Plaza jana  Jumamosi, akiongoza  umati  wa  watu  kwa kuahidi  kuendeleza  mapinduzi.

"Mbele  ya  mabaki  ya  mwili  wa  Fidel .. tunaapa  kulinda  ardhi  ya baba  zetu  na  ujamaa," Raul  Castro  alisema. "Ameonesha kwamba , ndio tutaweza, ndio  tunaweza, ndio tutavuka  vikwazo vyovyote, kitisho, misukosuko  katika  nia  yetu  thabiti  kujenga ujamaa  nchini  Cuba," alisema.

Alama za kuabudiwa

Castro  aliyefariki  Novemba  25  akiwa  na  umri  wa  miaka  90 atazikwa , katika  tukio  "dogo  la kawaida"  karibu  na  kaburi  la shujaa  wa  uhuru  wa  karne ya  19   Jose Marti, Castro  alisema.

Kuba Trauerfeier Fidel Castro
Wanajeshi na viongozi wa kitaifa wakitoa heshima za mwisho mbele ya majivu ya Fidel CastroPicha: Getty Images/AFP/R. Arangua

Lakini  bunge  la  taifa , ambalo  linakutana  baadaye  mwezi  huu, litaidhinisha  sheria  kutimiza ombi la  Castro  wakati  akifariki kwamba  hakutawekwa  sanamu  kwa  ajili  ya  kumbukumbu  yake ama   mtaa  ambao  utaitwa  kwa  jina  lake , alisema.

"Kiongozi  wa  mapinduzi  amekataa kila  aina  ya  kumtukuza," Raul Castro  alisema.

Wakati  Castro  alikaa  kanda  kwa  muda  mrefu  kutokana  na upasuaji  katika  utumbo muongo  mmoja  uliopita, ameendelea  kuwa mtu  muhimu  nchini  Cuba.

Aliheshimiwa na  waungaji  wake  mkono  kutokana  na  kutoa matibabu  bure  pamoja  na  elimu  bure  aliyoisambaza  katika kisiwa  hicho, na  alichukiwa  na  wapinzani  ambao  walimuona kama  dikteza  katili.

Santiago de Cuba Trauerfeier Fidel Castro
Bango lililoandikwa maneno "Mimi ni Fidel" mjiniSantiago de CubaPicha: Reuters/E. De La Osa

Huzuni na  masikitiko

Mazishi  yake  yanakamilisha  kipindi  cha  siku  nne  za  maombolezi ambamo Wacuba , mara  kadhaa  wakihamasishwa  na  serikali, walimiminika  mitaani  kutoa  heshima  zao  kwa  Castro, wakiimba "mimi  ni  Fidel" wakati  majivu  ya  mwili  wake  yakichukuliwa  kupita katika  nchi  hiyo  kuelekea  katika  mazishi.

"Nina  masikitiko  makubwa  kwasababu  tumempoteza  baba," alisema  marta Loida , profesa  wa  chuo  kikuu  mwenye  umri  wa miaka 35 akiwa  amekaa  chini  akishikilia  picha  ya  Fidel Castro baada  ya   hotuba  ya  Raul.

"Ni kama  hatutaki  kusema  kwaheri," amesema . "Tunataka kuendelea  kuwa  nae usiku  kucha  chini  ya  nyota."

Kubanischer Präsident Raul Castro
Raul Castro mdogo wake marehemu Fidel Castro , rais wa sasa wa CubaPicha: Reuters/C. Barria

Serikali  ililea hamasa  hii  ambayo imekuwa  kama  ya  kidini, huku vyombo  vya  habari  vya  serikali  vikimuita  Castro  "kamanda  wa milele."

Katika  wiki  moja  iliyopita , Wacuba  walihimizwa  kwenda  shuleni na  maeneo  mengine  ya  majengo  ya  umma kutia  saini  kiapo  cha kuwa  watiifu  kwa  mapinduzi  yake.

"Namuamini  Raul  kwasababu  Raul  ni  kaka  yake  Fidel. Fidel alimfundisha  kila  kitu,"  alisema  Irina Hierro Rodriguez, mwalimu mwenye  umri  wa  miaka  23  katika  mkutano  wa  Jumamosi.

Fidel Castro Asche in Santiago de Cuba
Ummati wa watu wakibeba mabango yenye icha ya Fidel Castro mjini Santiago de CubaPicha: Reuters/C. Barria

Licha  ya  kuwa  Raul Castro  alitoa  ahadi  kama  hiyo, ametekeleza mageuzi  kiasi  ya  kiuchumi  katika  miaka  ya  hivi  karibuni, akirejesha  uhusiano  wa  kidiplomasia  na  Marekani  na  kuapa kwamba  atajiuzulu  mwaka  2018.

"Akiwa hayuko  tena  chini  ya  kivuli  cha  kaka  yake , Raul  huenda sasa  akajihisi  kuwa  huru  zaidi  kuendelea  na  mageuzi  ya kiuchumi  aliyoyaanzisha  muongo  mmoja  uliopita," alisema Jorge Duany, mkurugenzi  wa   taasisi  ya  utafiti  ya  Cuba  katika  chuo kikuu  cha  kimatifa   cha  Florida nchini  Marekani.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Isaac Gamba