1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDU kuchagua mwenyekiti wa chama kumpokea Merkel

Yusra Buwayhid
7 Desemba 2018

Masaa kadhaa kabla ya kufanyika kwa mkutano wa chama cha Christian Democratic Union (CDU) wa kumchagua mwenyekiti mpya wa chama atakaempokea Angela Merkel, muungano wa kihafidhina umeongeza uungwaji mkono.

https://p.dw.com/p/39dHm
US-Magazin Forbes kürt Merkel zur mächtigsten Frau des Jahres
Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Wajumbe 1,001 wa chama cha CDU watakuwa na kibarua cha kumchagua mwenyekiti mpya wa chama na viongozi wengine wa ndani ya chama, katika mkutano wa siku mbili unaoanza Ikumaa huko mjini Hamburg. Halikadhalika, watakuwa wanajiandaa kumsaka mtu wa kusimama kama mgombea wa chama hicho katika nafasi ya ukansela, kwa ajili ya siku za baadae pale muda wa uongozi wa Angela Merkel utakapomalizika.

"Nimekuwa kiongozi wa chama kwa miaka 18, huo ni muda mrefu. Katika kipindi hicho, chama cha CDU kilipitia misukosuko na mafanikio tofauti.  Lakini chama pia kilipata wingi wa kura mara nne kufuatia chaguzi kuu. Na kwa hilo, lazima tuwashukuru wapiga kura, " alisema Merkel kabla ya mkutano huo wa CDU, alipokuwa akikagua eneo utakapofanyika mkutano.

Katika utafiti mpya wa maoni ya raia uliochapishwa Alahamisi na shirika la habari la Ujerumani la ARD, chama cha CDU pamoja na chama ndugu cha jimbo la Bavaria, Christian Social Union (CSU), vimeongeza uungwaji mkono kwa alama nne kufikia uungwaji mkono wa asilimia 30.

Deutschland CDU-Regionalkonferenz Düsseldorf l Merz, Kramp-Karrenbauer und Spahn
Wagombea wa uwenyekiti wa CDU Friedrich Merz, Annegret Kramp-Karrenbauer na Jens SpahnPicha: picture alliance/dpa/F. Gambarini

Kramp-Karrenbauer aongoza

Kama ilivyokuwa mwezi uliopita, asilimia 45 waliohojiwa katika utafiti wa maoni ya raia wanamuunga mkono  Annegret Kramp-Karrenbauer. Asilimia 30 wanamuunga mkono Friedrich Merz aliyekuwa kiongozi wa zamani wa muungano wa vyama vya kihafidhina katika bunge la Ujerumani. Na waziri wa Afya Jens Spahn anashika nafasi ya tatu akiwa na uungwaji mkono wa asilimia 10.

Kramp-Karrenbauer, ambaye kwa sasa ni mgombea anaeongoza katika kinyang'anyiro cha kumpokea Kansela Angela Merkel uongozi wa chama cha Christian Democtraic Union (CDU), amesema hapo jana kwamba chama hicho lazima kibaki kuwa na umoja bila kujali nani atakaeshinda kura ya leo Ijumaa ya kumchagua kiongozi mpya.

Merkel anapanga kuachia ngazi ya uwenyekiti wa chama cha CDU lakini atakabi kuwa kansela hadi uchaguzi wa mwaka 2021.

Wengi wa Wajerumani wanakubaliana na uamuzi wake huo. Hadi hivi sasa asilimia 57 ya watu waote waliohojiwa wanasema wanamtaka Merkel abaki madarakani kama kansela kwa miaka mengine mitatu hadi kutakapoitishwa uchaguzi mkuu. Asilimia 39 hata hivyo wanamtaka Merkel aachie ukansela kabla ya muda wake kumalizika.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW/AFPTV/dpa/

Mhariri: Caro Robi