1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yapinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa Monduli-Arusha

Charles Ngereza17 Septemba 2018

Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekataa matokeo ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Monduli kikidai kuwa uchaguzi huo ni haramu kwa kuwa ulitawaliwa na uvunjaji wa sheria.

https://p.dw.com/p/34yoi
Tansania Ersatzwahlen Wahlbeobachter in Arusha
Picha: DW/C. Ngereza

Jumapili (16.09.2018) nchini Tanzania kwa mara nyengine tena kulikuwa na uchaguzi wa marudio unaotokana na wabunge wa upinzani kuhama vyama vyao na kugombea kupitia chama tawala, CCM, na kwa mara nyengine chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, kimekataa matokeo ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Monduli kikidai kuwa uchaguzi huo ni haramu kwa kuwa ulitawaliwa na uvunjaji wa sheria kanuni za tume ya uchaguzi na hujuma kwa chama hicho. 

Mgombea wa uchaguzi huo kupitia Chadema, Yonas Laizer, alitoa msimamo huo katika mahojiano maalum na DW muda mchache baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa usiku wa kuamkia leo.

Julius Kalanga wa CCM atangazwa mshindi

Matokeo ya uchaguzi huo yanaonesha kuwa mgombea wa CCM, Julius Kalanga, alishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 95 ya kura zote zilizopigwa na Chadema kuambualia asilimia 5 tu.

Lakini Laizer anasema uchaguzi huo ulihujumiwa kwa kuwa baadhi ya mawaziri wa serikali walishiriki katika kampeni za uchaguzi huo na kuahidi kuwa endapo CCM kingelishinda, serikali yake ingeliwapelekea maendeleo na kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Maafisa wa polisi katika gari lao wakifanya doria kulinda usalama
Maafisa wa polisi katika gari lao wakifanya doria kulinda usalamaPicha: DW/C. Ngereza

Mgombea huyo alisema kuwa anakusanya ushahidi wa matukio yote ya uvunjifu wa kanuni na taratibu zilizovunjwa na wapinzani wao ili kuweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kulifikisha suala hilo mahakamani pamoja na hatua zingine ambazo alisema zitachukuliwa na wapiga kura wa jimbo hilo.

Madai ya mawakala wa Chadema kutekwa.

Kauli ya mgombea huyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa baraza la vijana na la taifa la chama hicho Patrtick Ole Sosopi, ambaye alidai kuwa kuwa mawakala wa chama chake walitekwa na wengine kupigwa huku gari la mbunge wa chama hicho likishambuliwa na watu wasiojulikana wakati wakisambaza mawakala kwenye vituo.

Hata hivyo, chama tawala CCM kupitia meneja wa mgombea wake na aliyetangazwa mshindi, Wiliam Nasha, kimetupilia mbali madai ya Chadema na kusema kuwa ushindi wao umetokana na wananchi kukikubali chama hicho.

Kwa upande wake Jeshi la polisi limesema kuwa uchaguzi huo umefanyika kwa amani na kutupilia mbali madai ya mawakala wa CHADEMA kutekwa kwa kuwa hakuna tukio lolote liliripotiwa polisi isipokuwa la mbunge wa viti maalum wa Chadema ambaye gari lake lilishambuliwa na magurudumu yote manne kutobolewa na watu wasiojulikana.

Mhariri: Mohammed Khelef