1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yasusia chaguzi za marudio

Mohammed Khelef
19 Septemba 2018

Siku mbili baada ya kushindwa chaguzi, chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimetangaza kususia chaguzi ndogo kwa madai ya kukosekana kwa uadilifu kwenye mamlaka za kuendesha na kusimamia chaguzi hizo.

https://p.dw.com/p/35AM2
Tansania Chadema-Parteivorsitzender Freeman Mbowe 
Picha: DW/E. Boniphace

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao ya chama chake jijini Dar es Salaam hivi leo (Septemba 19), Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kamati kuu imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa "hakuna haja ya kushiriki chaguzi ambazo haziheshimu maamuzi ya wananchi."

Akizungumzia kile alichokiita hujuma za wazi za maafisa wa Tume ya Uchaguzi (NEC), polisi, jeshi la usalama wa taifa, na viongozi wa serikali ngazi za wilaya na mikoa, Mbowe alisema "kumekuwa na 'militarisation' (zoezi la kijeshi) ya mchakato wa uchaguzi."

"Imani ya wananchi kwenye sanduku la kura imefifia. Kura haiamui tena nani ashikilie nafasi ya uwakilishi wa wananchi. Tunashuhudia kauli ya Rais Magufuli ikiwa ndio kila kitu," alisisitiza Mbowe.

Kauli hii ya CHADEMA inakuja siku mbili baada ya chama chake kushindwa vibaya kwenye chaguzi nyengine mbili za marudio katika nafasi ya ubunge kwa majimbo ya Monduli na Ukonga, yote yakiwa ngome zake.

Tangu kutangazwa kwa matokeo ya chaguzi hizo, ambazo wagombea wa CCM wametajwa kuwa washindi, kumeibuka mjadala mkali baada ya vidio iliyosambazwa mtandaoni kumuoyesha mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akishangiria na kupongezana na askari wa jeshi la polisi kutokana na ushindi huo wa chama tawala, huku wadadisi wakisema tukio hilo linaashiria jinsi vyombo vya dola vinavyotumiwa kuhakikisha ushindi kwa chama kilicho madarakani.

Mbali ya vyama vya siasa, pia makundi yanayojipambananua kama watetezi wa demokrasia yamekuwa yakiilaumu tume ya uchaguzi ya nchi hiyo na hivi karibuni yalipitisha mapendekezo ya kutaka tume hiyo ifanyiwe marekebisho kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao wa 2020.

Lakini licha ya kukosolewa kuegemea upande wa watawala, tume hiyo imekuwa zikisisitiza kwamba inatenda kazi zake kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazowaongoza, na kwamba mapungufu ya upinzani ndio msingi wa kupoteza kwake kwenye chaguzi.

Kauli kama hiyo hutolewa pia na chama tawala, CCM, ambacho katika mikutano yake ya mara kwa mara na waandishi wa habari kimekuwa kikisema kuwa ushindi wake kwenye chaguzi zote za marudio "unatokana na namna kinavyozidi kukubalika kwa wananchi, hasa kutokana na kazi ya Rais Magufuli."

Chaguzi ambazo zinagomewa na CHADEMA kwa sasa ni pamoja na ule wa Liwale, kusini mwa nchi hiyo, na nyengine za vitongoji na vijiji 37, nyingi zao zikitokana na wawakilishi kutoka vyama vya upinzani kujiuzulu nafasi zao na kujiunga na chama tawala, CCM, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni "kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli" katika kulijenga taifa hilo kubwa Afrika Mashariki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/George Njogopa
Mhariri: Lilian Mtono