1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanya unazidi kupanuka kati ya CDU na CSU

15 Machi 2016

Mada moja tu imehodhi vichwa vya magazeti ya Ujerumani hii leo; Zilzala ya kisiasa kufuatia uchaguzi katika majimbo matatu ya Ujerumani na mataokeo yake.

https://p.dw.com/p/1IDFr
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Tunaanzia na suala la hali ikoje katika chama cha Christian Democratic Union. Gazeti la "Rheinische Post" linaandika:"Chama cha CDU kimeingia ufa-na ufa huo umezidi kupanuka baada ya matokeo ya kuvunja moyo ya chama hicho katika chaguzi tatu za majimbo jumapili iliyopita. Kwa upande mmoja wanakutikana wale wanaomuunga mkono Merkel na upande wa pili wapo wale wanaompinga na vitisho vyao vinavyohanikiza. Pale mwenyekiti wa Christian Social Union-CSU-Horst Seehofer anapomtuhumu Merkel kuvitia hatarini vyama ndugu vya CDU-CSU,matamshi hayo yanamaanisha hayuko mbali na kutoa wito wa mapinduzi. Merkel hawezi tena kuvumilia miito kama hiyo. Wana CDU/CSU wanaonyesha wameingiwa na taharuki. Hali hiyo imezidi kutokana na tathmini potovu ya wenye kumuunga mkono Merkel. Kudai eti asili mia 80 wanaunga mkono sera ya Merkel kuelekea wakimbizi ni kujaribu kufifiisha madai ya wapiga kura. Kusema kansela hayuko mbali na kufikia ufumbuzi kwa daraja ya Ulaya ni hadaa. Kinachohitajika zaidi kwa sasa ni Ukweli,ufafanuzi na kutiliwa maanani wasi wasi wa wananchi na wale wanaomuuunga mkono Merkel.

Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linaangalia sababu zilizopelekea ushindi wa chama cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD na kuandika:"Chaguzi tatu za jumapili ziligeuka bila ya shaka chaguzi za malalamiko. Lakini kuna kila sababu zinazoonyesha suala la wakimbizi litapungua uzito wake miezi inayokuja. Merkel anavuta wakati. Pengine hilo haliridhishi. Lakini bila ya majadiliano ya dhati tatizo la wakimbizi haliwezi kutatuliwa ipasavyo. Na kila wakati ambapo juhudi za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya jamii zitakapoleta tija ndipo nazo juhudi za wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia zitakapokuwa kazi bure. Vyama vikuu visijiachie kuvunjika moyo na vikiendelea kuzozana kama hivi sasa,watakaofaidika si wengine isipokuwa AfD.

Karata zinachanganywa kuunda serikali ya muungano Stuttgart

Gazeti la "Mannheimer Morgen" linamulika juhudi za kuunda serikali katika jimbo la Baden-Wuerttemberg na kuandika:"Kutokana na matokeo namna yalivyo,kila kitu kinaashiria uwezekano wa kuundwa serikali ya walinzi wa mazingira die Grüne na Christian Democratic Union-CDU. Lakini CDU watalazimika kumeza machungu kwasababu wengi miongoni mwa wahafidhina wanaendelea kuwaangalia walinzi wa mazingira kama kitisho. Muungano wa aina hiyo utakuwa mtihani mkubwa kwa CDU. Kwa hivyo kila upande hivi sasa unajaribu kucheza karata zake. Ingawa hata katika karata mtu anaweza kuondolewa patupu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman