1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha AfD chapata viongozi wapya

24 Aprili 2017

Alexander Gauland na Alice Weidel ndio watakaoongoza juhudi za chama cha AfD kuingia katika bunge la Ujerumani katika uchaguzi mkuu wa Septemba 24.

https://p.dw.com/p/2bn9p
AfD Bundesparteitag Alice Weidel , Alexander Gauland
Alexander Gauland na Alice WeidelPicha: picture alliance/dpa/R.Vennenbernd

Hii ni baada ya wanachama wa chama hicho kuwachagua Jumapili, katika mkutano mkuu uliofanyika mjini Cologne. Gauland alikuwa mwanachama wa kitambo wa chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel na anajulikana kwa matamshi yake makali.

Idadi kubwa ya wanachama wa AfD waliwaunga mkono Gauland mwenye umri wa miaka 76 na Weidel aliye na miaka 38 ambaye ni mchumi aliyewahi kufanya kazi benki. Kuchaguliwa kwao kulifuatia tangazo lililowashangaza wengi la kiongozi mwenza wa chama hicho Frauke Petry, ambaye ni sura ya chama hicho, kwamba, hataongoza kampeni za chama hicho jambo ambalo huenda likawapa fursa ya ushindi vyama vyengine kama kile cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel.

Gauland ni mmoja wa wanachama walio na ushawishi mkubwa katika chama hicho na ni mmoja wa wapinzani wakuu wa Petry, ila alisema Petry bado anahitajika AfD.

Gauland anasema Merkel lazima aondolewe madarakani

"Hili lilikuwa ni kongamano lenye ufanisi, kongamano zuri na tumemshukuru kila mmoja aliyehusika katika maandalizi yake," alisema Gauland. "Lakini rafiki zangu, halikuwa kongamano rahisi, na jana ilikuwa siku ngumu. Mpendwa Frauke Petry, najua ulikuwa na siku ngumu jana, lakini tunakuhitaji katika chama," aliendelea kusema Gauland.

Deutschland AfD Bundesparteitag in Köln
Wanachama wa AfD katika mkutano mkuu wa chama, mjini ColognePicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Gauland alisema Kansela Merkel ambaye AfD inamtuhumu kwa kuwakubalia wahamiaji zaidi ya milioni moja kuingia nchini Ujerumani katika miaka miwili iliyopita, ni lazima aondolewe madarakani.

Kuchaguliwa kwa wawili hao kunakiweka chama cha AfD katika njia ambayo wengi hawakuitaraji hata juma moja lililopita, ambapo ilifikiriwa kwamba Petry angekuwa mmoja wa watu ambao wangekuwa mstari wa mbele kukiongoza chama hicho kuelekea bungeni. Kulikuwa na uvumi pia kwamba alikuwa anataka kuongoza harakati hizo peke yake, lakini alisema Jumatano kwamba hatoshiriki kura.

Petry amekuwa akikitaka AfD kulegeza msimamo kuhusiana na wakimbizi

Petry pia amekuwa akikishinikiza chama cha AfD kulegeza msimamo wake kuhusiana na kupinga suala la uhamiaji, jambo ambalo limekuwa kama kitambulisho cha chama hicho, lakini wanachama walilipinga hilo wazo lake katika kongamano hilo na kushindwa katika azma yake hiyo, kunaelezea kuwa huenda pia ikawa sababu ya Petry kujitenga na kampeni za chama hicho.

Köln AfD Parteitag Frauke Petry
Frauke Petry wa AfDPicha: Getty Images/S. Schuermann

"Kwa maoni yangu, iwapo wangelikubalia wazo hilo, lingekisaidia chama cha AfD kuamua mkakati wake kama ulivyopendekezwa ili kutoa nafasi ya wapiga kura zaidi na pia ni suala ambalo lingeweka wazi mipaka iliyoko," alisema Petry. "Hii ni tofauti kubwa kwa mfano na chama cha Marine Le Pen, kwani amefanya hivi tangu mwaka 2011 ambapo hata alimtimua chamani babake mwenyewe, na unaweza kuona chama cha France National kilinufaika katika matokeo ya uchaguzi," alimaliza Petry.

Katika kongamano hilo wanachama pia walipigia kura manifesto ya chama ambayo imeweka sheria kali kwa wahamiaji na Waislamu na inazungumzia pia kujiondoa kwa Ujerumani katika sarafu ya Yuro. Mkuu wa Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani Joseph Schuster amekishutumu AfD kwa hatua hiyo akisema, chama hicho kinawatishia Wayahudi na Waislamu nchini Ujerumani.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/APE/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga