1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha ANC chaanza kumchagua kiongozi mpya

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CciQ

Wanachama zaidi ya 4,000 wa chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, wameanza kupiga kura hii leo kumchagua kiongozi mpya wa chama hicho. Rais Thabo Mbeki anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa hasimu wake bwana Jacob Zuma.

Rais Thabo Mbeki amesema ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na migawanyiko ndani ya chama ni mambo yanayotishia kukiharibu chama cha ANC, ambacho kimekuwa kikitawala Afrika Kusini tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi mnamo mwaka wa 1994.

´Kama tumegawanyika, je tunatakiwa tufanye nini ili tuweze kukabiliana na changamoto hii, tukizingatia ukweli ulio wazi kwamba chama cha ANC kilichogawanyika hakiwezi kutimiza wajibu wake wa kihistoria kwa wananchi wetu.´

Kushindwa kwa rais Mbeki katika uchaguzi huo huenda kukawa pigo kubwa kwa serikali yake huku ikiwa imesalia miaka miwili kabla awamu yake ya urais kumalizika.

Hata hivyo kwa bwana Zuma utakuwa ni ushindi mkubwa kwa mtu aliyefutwa kazi alipokuwa makamu wa rais mnamo mwaka wa 2005 baada ya mshauri wake wa maswala ya fedha kuhukumiwa kifungo gerezeni kwa kuhusika na vitendo vya rushwa.