1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha ANC chaanza kumchagua kiongozi mpya

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Ccrv

Mkutano wa baraza kuu la chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini umejaribu kumaliza mashindano makali ya kuwania uongozi wa chama hicho hii leo.

Wanachama zaidi ya 4,000 wa chama cha ANC, wanaanza kupiga kura leo kumchagua kiongozi mpya.

Rais Thabo Mbeki anatarajiwa kushindwa na mpinzani wake mkubwa bwana Jacob Zuma, ambaye ni naibu mwenyekiti wa chama.

Rais Mbeki amesema ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na migawanyiko ndani ya chama ni mambo yanayotishia kukiharibu chama cha ANC, ambacho kimekuwa kikitawala Afrika Kusini tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi mnamo mwaka wa 1994.

´Kama tumegawanyika, je tunatakiwa tufanye nini ili tuweze kukabiliana na changamoto hii, tukizingatia ukweli ulio wazi kwamba chama cha ANC kilichogawanyika hakiwezi kutimiza wajibu wake wa kihistoria kwa wananchi wetu.´

Kushindwa kwa rais Mbeki katika uchaguzi huo kutakuwa pigo kubwa kwa serikali yake huku ikiwa imesalia miaka miwili kabla awamu yake ya urais kumalizika.

Hata hivyo kwa bwana Zuma utakuwa ni ushindi mkubwa kwa mtu aliyefutwa kazi alipokuwa makamu wa rais mnamo mwaka wa 2005 baada ya mshauri wake wa maswala ya fedha kuhukumiwa kifungo gerezeni kwa kuhusika na vitendo vya rushwa.